BASATA Yaunga Mkono Ubunifu wa Madee na Fid Q

 



KAIMU Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Edward Buganga amepongeza na kuunga mkono ubunifu wa wanamuziki nguli nchini Hamadi Ali ‘Madee’ na Farid Kubanda ‘Fid Q’ kwa kuanzisha programu itakayoleta chachu kwa wanamuziki wa zamani kuungana kufanya kazi kwa pamoja. Aidha, Buganga amewasisitiza wasanii na jamii yote kuwapokea wanamuziki hao ili waweze kuipeleka ajenda ya umoja na ubunifu katika maisha ya kila siku kuwa msingi wa maendeleo endelevu.

Alisema muziki unatoa burudani na kukuza kipato hivyo amewaasa wadau kuwa sehemu ya ushiriki wa tamasha hilo litakalofanyika Julai 10, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Aliongeza kuwa enzi zao maudhui ya Bongo fleva yalifanywa kwa kuzingatia maadili, hivyo amewataka wadau na wanamuziki kuwaunga mkono wasanii hao ili warudishe umoja na ubunifu wa zamani.

Naye Madee alisema wanamuziki wanaoshiriki tamasha hilo waliongozwa na ndoto ya matumaini kwa miaka 30 yenye vikwazo vingi kuaminisha wadau na wananchi kuwa muziki ni ajira inayoweza kutanua wigo wa kipato kwa wasanii. Alisema mwanzoni mwa miaka ya 1990 walipata changamoto kubwa ya kuonekana muziki wao unafanywa na wahuni kutokana na mavazi na makundi kutengeneza maudhui yenye kuibua changamoto za kijamii zinazoshindwa kuelezwa kikawaida katika majukwaa mengine.

Kutokana na hali hiyo, wanamuziki walijikita kutoa nyimbo zilizoelezea ndoto na matamanio ya jamii kwa kuzingatia ulinzi wa maadili ya Kitanzania. Aliongeza kuwa, kwa sasa muziki umeingia katika mfumo wa biashara na wasanii na wadau wa sanaa wanapata kipato, lakini kuna shughuli kubwa ya kulinda maadili, hivyo wanafanya tukio hilo kuwaonesha ramani bora wasanii kulinda maadili ya Kitanzania.

Mkurugenzi wa Ubunifu wa tamasha hilo Fid Q ameweka wazi kuwa tamasha hilo litatanguliwa na semina elekezi kwa wasanii na wadau wa sanaa itakayotolewa na wataalamu wabobezi kwenye biashara na uchumi, hivyo kutanua wigo wa soko la kazi za muziki ndani na nje ya nchi. Alihitimisha kwa kueleza kuwa muziki ukiandaliwa kwa vionjo vyenye asili ya Kitanzania na kutumika vizuri utasaidia kueneza utamaduni na mkong’osio wake katika mataifa mbalimbali.

No comments