WACHINA WANNE MBARONI KWA TUHUMA ZA KUTEKA WENZAO NA KUDAI DOLA MILIONI 20
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata raia wanne wa China kwa tuhuma za kuhusika na tukio la utekaji wa wafanyabiashara wenzao wawili jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo lilitokea Mei 14, 2026 majira ya saa 4:30 usiku katika majengo ya PSSSF yaliyopo Mtaa wa Mission, Ilala, ambapo watu wawili waliotajwa kuwa ni Weiyi Chen (64) na Liang Xiolo (44), wote wafanyabiashara na raia wa China, walidaiwa kuvamiwa na kutekwa na kundi la watu saba na kupelekwa kusikojulikana.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi lilianza ufuatiliaji na kufanikiwa kubaini magari yaliyodaiwa kutumika katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amesema miongoni mwa magari yaliyokamatwa ni Toyota Alphard lililokuwa na namba T.305 DRP ambazo zimedaiwa si halali kwa gari hilo pamoja na Toyota Harrier lenye namba T.188 DHT.
Amesema watuhumiwa hao walitoa vitisho kwa ndugu wa mateka wakitaka walipwe dola za Marekani milioni 20 ili kuwaachia.
Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwaokoa mateka hao Mei 16, 2026 katika eneo la Mbezi, Kinondoni, ambapo walikutwa wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Deng Anqing (49), Fan Zhong (49), Zhang Jianjun (51) na Deng Qiang (40), wote raia wa China.
Polisi wamesema watuhumiwa hao walikutwa na simu za mateka hao pamoja na vielelezo vingine vinavyohusishwa na tukio hilo, na kwamba linaendelea kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo na kila atakayebainika kuhusika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Post a Comment