RAIS DKT. MWINYI ASITISHA MJADALA WA KUONGEZA MUDA WA URAIS
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema hana nia ya kuongeza muda wa Urais zaidi ya muda uliowekwa kikatiba na kuagiza kusitishwa mara moja kwa mijadala kuhusu suala hilo.
Dkt. Mwinyi amesema kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo Baraza la Wawakilishi, kumekuwa na mijadala na mapendekezo ya kuongeza muda wa Urais badala ya miaka 10 iliyowekwa na Katiba ya Zanzibar, lakini amesisitiza kuwa hana dhamira hiyo na kwamba mjadala huo hauna tija kwa nchi kwa sasa.
Amesema viongozi wameapa kuilinda Katiba ya Nchi na kuwataka wananchi na viongozi kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa maendeleo ya taifa. Ameeleza kuwa kipindi kilichobaki cha uongozi wake kitakuwa cha utekelezaji mkubwa na wa kasi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 23 Mei 2026 alipofungua Jukwaa la Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma lililofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali haitakuwa tayari kuendelea kubeba mashirika ya umma yanayoshindwa kujiendesha na kuendelea kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.
Amesema bado yapo mashirika ya umma yanayolipwa mishahara na kuendeshwa kwa fedha za Serikali jambo alilosema limepitwa na wakati, huku akiitaka taasisi hizo kujipanga na kujiendesha kwa tija na faida.
Halikadhalika Dkt. Mwinyi amesema Serikali itatoa muda kwa mashirika hayo kufanya mageuzi ya kiutendaji na yale yatakayoshindwa kujiendesha Serikali haitakuwa tayari kuendelea nayo.
Vilevile Dkt. Mwinyi amesisitiza kuendelea kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi na uimarishaji wa bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo na miundombinu ya barabara ili kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uchumi wa kisasa na endelevu.

Post a Comment