HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YASAKA SHILINGI BILIONI 7 KUFANIKISHA TIBA YA UPANDIKIZAJI FIGO NA ULOTO KWA WATOTO




Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inahitaji kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya ubingwa bobezi ya upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu pamoja na upandikizaji wa figo kwa wananchi wenye uhitaji mkubwa wa huduma hizo. 

Mahitaji haya yametangazwa leo tarehe 21 Mei 2026 katika Ukumbi wa NIMR Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi katika mkutano wake na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri, Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Miitandao Tanzania  (JUMIKITA).

Alisema kwa sasa kuna watoto 50 wanaohitaji upondikizaji wa uloto na wengine 50 kwa ajili ya upandfikizaji wa figo.

Mkutano huo ni sehemu ya  maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, hapo Julai 15 ,2026 ambapo safari ya maadhimisho haya ilizinduliwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2025. 

Tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo  Oktoba 13,2015, Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa na dhamira ya kutoa huduma za kibingwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kuzuia, kuchunguza, na kutibu magonjwa mbalimbali, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya tafiti. 

Kwa sasa, BMH inahudumia takribani wananchi milioni 10 kutoka mikoa nane ya Tanzania, ikiwa na vitanda 400 na watumishi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa na bingwa bobezi zaidi ya 100. 

Kwa mujibu wa Profesa Makubi Hospitali hiyo inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma 18 za ubingwa bobezi zikiwemo upandikizaji wa viungo, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, huduma za radiolojia ya kisasa, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, upasuaji wa njia ya matundu madogo, pamoja na uchujaji wa damu.

Profesa Makubdi amesema ndani ya miaka  10 ya utendaji, hospitali imepata mafanikio makubwa yaliyochangiwa na uwekezaji wa serikali katika miundombinu na vifaa vya kiasi cha shilingi bilioni 283, huku idadi ya watumishi ikiongezeka kutoka 20 tu mwaka 2015 hadi kufikia 1,076 mwaka 2026.

Hospitali imefanikiwa kupanua na kuboresha huduma za matibabu ya kibobezi, ikiwemo uanzishwaji wa huduma muhimu za upandikizaji figo na uloto kwa watoto wenye selimundu, pamoja na kukuza tiba utalii kwa kuhudumia wagonjwa wa kigeni na viongozi mashuhuri, wakiwemo wagonjwa 2,897 kutoka Burundi, 526 kutoka Comoro, na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 

Ubora wa huduma umeongezeka kupitia upasuaji wa matundu na uanzishwaji wa Kliniki ya Kifalme (Royal Clinic) mnamo tarehe 10 Julai 2025, ambayo imeshalaza na kuhudumia wagonjwa 18,607, wakiwemo wagonjwa wa kimataifa 390 waliofanyiwa uchunguzi mkubwa wa afya (Master Health Check-up). 

BMH pia imepata ithibati ya kimataifa ya maabara ya ISO 15189:2022, imeboresha mifumo yake ya TEHAMA, imeweka mfumo wa kisasa wa kuelekeza wagonjwa (queuing system) na kutoa maoni, na imefanikiwa kupunguza muda wa mgonjwa kusubiri huduma kutoka wastani wa saa 8 hadi saa 3 tu.

"Tunatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na hasa ndani ya BMH, na ninatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kuokoa maisha ya wagonjwa huku sisi tukiahidi kuendelea kuishi kwa kauli mbiu yetu ya kuvaa viatu vya mgonjwa, uwajibikaji, na kujituma, " alisema Profesa Makubi.

Katika kuimarisha miradi ya kimkakati, hospitali inaendelea na ujenzi wa jengo la matibabu ya saratani lenye thamani ya shilingi bilioni 32, jengo la matibabu ya figo la shilingi bilioni 44.9 linalojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Japani iliyochangia bilioni 28 na Serikali ya Tanzania iliyochangia bilioni 16.9, uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha upandikizaji uloto, pamoja na chuo kinachotoa elimu ya ngazi ya Stashahada. 

Akizungumzia mwelekeo Preofesa Makubdi alisema taasisi hiyo kwa miaka 10 ijayo inajipanga kubobea zaidi na kuwa kijiji cha utalii wa matibabu katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma. 





Kuelekea kilele cha tarehe 15 Julai 2026, matukio mbalimbali yamepangwa na mengine tayari yamefanyika ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau, ikiwemo mikutano iliyofanyika mwezi Aprili 2026 jijini Dar es Salaam na Arusha na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote za Umma, ambapo takriban shilingi bilioni 4 zimeshapatikana kutoka kwa wadau wa sekta ya umma na kampuni zenye ubia na serikali. 

Aidha, Kongamano la Kisayansi lililoangazia hali ya huduma za upandikizaji viungo nchini lilifanyika tarehe 6 Mei 2026 katika Ukumbi wa Domiya Estate likishirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi, na hivi sasa maandalizi ya dhifa za chakula cha jioni (Gala dinners) pamoja na mbio maalumu za Marathon yanaendelea ili kuchangisha fedha hizo.

Zoezi hili la harambee la kusaidia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na figo linafanyika kwa kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kuwasaidia Watanzania wasio na uwezo ambao idadi yao inaongezeka kila siku. 

Harambee hiyo kubwa itakayofanyika tarehe 15 Julai 2026 jijini Dodoma, inatarajiwa kuongozwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Profesa makubdi ameyaomba Mashirika, taasisi, makampuni, wadau, na wananchi wote  kuchangia kupitia njia rasmi zilizowekwa ambazo ni namba ya malipo (Control Number) 986930000001 au kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa akaunti namba 102501000407 zote zikiwa kwa jina la BMH Organ Transplant. 


No comments