BUNGE LASIFIA JUHUDI ZA RAIS SAMIA KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake madhubuti za kuhakikisha nchi inabaki katika hali ya amani na utulivu tangu alipoingia madarakani.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa kumshukuru Rais wa Kenya, Dk. William Ruto, kufuatia hotuba yake, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alibainisha kuwa Rais Samia ameonesha uongozi wa kipekee kwa kuwarudisha nchini wapinzani waliokuwa wamekimbilia nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa Rais Samia hakurudisha tu wanasiasa hao, bali pia alilipa madai ya watu mbalimbali kwa serikali ili kuondoa chuki na kujenga taifa lenye mwelekeo mmoja, jambo linalodhihirisha moyo wa dhati wa kutaka Tanzania moja kupitia falsafa yake ya 4R.
Spika Zungu aliongeza kuwa kielelezo kingine cha maono ya Rais Samia katika ujenzi wa taifa moja ni uamuzi wake wa hivi karibuni wa kumteua Dk. Eveline Munisi kutoka chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Spika alitoa wito kwa viongozi wa dini na wananchi wote kushirikiana na Rais kwa kuweka maslahi ya taifa mbele, akibainisha kuwa jitihada hizo za kufungua milango ya fursa na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni kielelezo cha uongozi uliotukuka. Aidha, alimshukuru Rais Ruto kwa hotuba yenye kujenga umoja na kuimarisha uhusiano wa kihistoria baina ya Kenya na Tanzania.
Kwa upande wao, wabunge mbalimbali walipata nafasi ya kutoa shukrani, wakisisitiza kuwa ushirikiano unaoonekana sasa unaleta matokeo chanya kwa wananchi wa mataifa yote mawili. Waziri Palamagamba Kabudi na Mbunge Anne Kilango Malecela walieleza kuwa hotuba ya Rais Ruto imebeba maono ya ushirikiano ambayo pia yanatekelezwa na Rais Samia kwa upande wa Tanzania. Vilevile, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, na Mbunge Elibariki Kingu walibainisha kuwa kazi zinazofanywa na viongozi hawa wawili ni mwendelezo wa ndoto za waasisi wa mataifa haya, Mwalimu Julius Nyerere na Jomo Kenyatta, na zitakumbukwa na vizazi vijavyo.
Post a Comment