YERICKO NYERERE AHIMIZA MARIDHIANO JUMUISHI YA KITAIFA KUELEKEA KATIBA MPYA



Kada wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Yericko Nyerere, ametoa mtazamo wake kufuatia ripoti ya Tume ya Jaji Chande akisisitiza kuwa mchakato wa maridhiano unaokuja haupaswi kuwa wa wanasiasa pekee bali unapaswa kuigusa jamii nzima ya Watanzania. 

Nyerere anaamini kuwa tume hiyo imefungua njia ya kuelekea kwenye ukweli kwa kuweka mwangaza juu ya vyanzo vya matukio mbalimbali na kutoa fursa kwa kila mhusika kuwajibika, isipokuwa tu kwa yale masuala yenye mwelekeo wa kijinai ambayo yanahitaji mkono wa sheria.

Anabainisha kuwa umuhimu wa maridhiano haya upo katika uwezo wake wa kutengeneza umoja wa kitaifa kwa kuwashirikisha wadau wote wakiwemo wakulima, wafugaji, na wafanyabiashara ambao kwa namna moja au nyingine wameguswa na hali ya mambo nchini. 

Kwa mujibu wa Nyerere, maridhiano si jambo la watu binafsi bali ni hitaji la kijamii linalolenga kutibu makovu ya nyuma ili taifa liweze kusameheana na kusonga mbele kwa pamoja kama kitu kimoja.

Aidha, mwanasiasa huyo ameeleza kuwa siasa zilizokomaa na zilizobalehe ni zile zinazotoa nafasi ya kuzungumza na kukubaliana katika mambo ya msingi kwa manufaa ya nchi. 

Anasisitiza kuwa tija kubwa ya maridhiano hayo itakuwa ni kuweka msingi imara wa kukubaliana juu ya hitaji la Katiba Mpya, kwani kupitia mazungumzo na maelewano, ni rahisi zaidi kufikia muafaka wa jinsi ya kuendesha nchi na kuzuia migogoro ya baadaye kupitia sheria mama ya nchi.

No comments