Uingereza Yaongoza Kwa Mitaji Tanzania na Soko la Hisa Likipaa
Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025 imebainisha kuwa nchi ya Uingereza imeshika nafasi ya kwanza kwa kuingiza Uwekezaji wa Moja kwa Moja Kutoka Nje (FDI) hapa nchini jambo linaloashiria kuongezeka kwa imani ya mataifa makubwa kwa uchumi wetu.
Takwimu hizi zilizokusanywa kwa ushirikiano wa Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA) pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonyesha kuwa Uingereza imewekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 499.8.
Ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na upanuzi wa biashara za kimkakati katika sekta za madini, huduma za fedha na bima, viwanda vya uzalishaji pamoja na sekta ya habari na mawasiliano.
Mataifa mengine yaliyofuata kwa karibu katika chati hiyo ya uwekezaji ni pamoja na Afrika Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu na China ambazo kwa pamoja zimeendelea kuwa washirika muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.
Uchambuzi wa kina wa ripoti hiyo unaonyesha kuwa uwekezaji huo umejikita katika maeneo yenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya muda mrefu ambapo nchi kumi zinazoongoza zimechangia takribani asilimia 64.7 ya uwekezaji wote wa mwaka 2024.
Moja ya sababu kuu zilizoifanya Uingereza kuongoza ni hatua ya ununuzi wa hisa kwenye sekta ya madini ambazo awali zilikuwa zikimilikiwa na wanahisa kutoka Canada na Visiwa vya Cayman.
Ingawa nchi ya Mauritius imekuwa ikiongoza kwa muda mrefu hali ilibadilika kidogo mwaka huu kutokana na urejeshaji wa mikopo ya kibiashara lakini ripoti inasisitiza kuwa hali hiyo haimaanishi kupungua kwa nia ya uwekezaji kutoka nchi hiyo. Kwa sasa Uingereza inashikilia asilimia 26.9 ya limbikizo lote la uwekezaji nchini ikifuatiwa na Mauritius na Norway jambo linaloonyesha kuwa Tanzania ina wigo mpana na wa aina mbalimbali wa vyanzo vya mitaji ya kigeni.
Sambamba na uwekezaji wa moja kwa moja soko la mitaji nchini nalo limeonekana kushamiri ambapo ushiriki wa wawekezaji wa kigeni katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) umeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Thamani ya soko hilo imepaa na kufikia Dola za Marekani bilioni 6.9 mwaka 2024 ikilinganishwa na Dola bilioni 6.1 za mwaka uliopita huku uwekezaji wa hisa ndogo ukiongezeka mara tano zaidi.
Aidha mahusiano ya kibiashara nje ya mipaka yameimarika kupitia mikopo ya kibiashara ya muda mfupi ambayo ilifikia Dola milioni 257.7 na kuelekezwa zaidi kwenye miradi ya uchimbaji madini na huduma za fedha. Maendeleo haya ya kitakwimu yanathibitisha kuwa mazingira ya biashara nchini Tanzania yanaendelea kuwa tulivu na yenye tija na hivyo kutengeneza fursa nyingi zaidi kwa ajili ya ukuaji wa viwanda na ustawi wa kijamii kwa siku za usoni.

Post a Comment