Knockout ya Mama Msimu wa Nane ni Kesho Ubungo EACLC




Mapambano ya msimu wa nane ya Knockout ya Mama yanatarajiwa kufanyika kesho katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam. 

Tukio hili linakuja baada ya kuahirishwa kwa wiki moja kutoka tarehe ya awali ya Aprili 24 mwaka huu kutokana na changamoto za kiafya zilizowapata baadhi ya mabondia waliopangwa kupanda ulingoni.

Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Udhibiti wa Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) Jacob Mbuya amesisitiza kuwa uamuzi huo wa kuahirisha mchezo ulilenga kulinda afya na usalama wa wachezaji huku Promota wa Mafia Boxing Promotion, Anatoly Nyaki akiwaomba radhi mashabiki kwa usumbufu uliojitokeza na kuwahakikishia kuwa maandalizi ya ziada yamekamilika kwa ajili ya tukio la kesho.

Hamasa ya mashabiki na wadau wa ngumi nchini inatarajiwa kuwa kubwa katika mapambano ya kesho Ijumaa yakiongozwa na pambano la ubingwa wa Shirikisho la Ngumi Dunia (WBO) Afrika ambalo ndilo litakalokuwa kivutio kikuu cha siku. 

Bondia Ibrahim Mafia ambaye ni mmoja wa washiriki wakuu ameeleza kujiamini kwake na kusema kuwa amejipanga kikamilifu kutoa onyesho la kusisimua na lenye kiwango cha juu. 

Aidha bondia huyo ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia mtanange huo ambao unatarajiwa kuwa na msisimko wa kipekee baada ya kusubiriwa kwa hamu kufuatia mabadiliko ya ratiba.

No comments