ZAIDI YA WANANCHI 180 WANUFAIKA NA MATIBABU YA BURE DAR ES SALAAM



Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Bingwa ya MDM Urology, Deogratius E. Mahenda, na Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Afya Nyumbani cha Nilax, May C. Moshatsi, kwa nyakati tofauti wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha programu za elimu ya afya kwa jamii na kupanua wigo wa vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza ili kusaidia utambuzi wa mapema na kuokoa maisha ya wananchi.

Wametoa kauli hizo baada ya kuhitimishwa kambi maalum ya matibabu ya siku mbili iliyolenga kusogeza huduma za afya karibu na jamii ilizyofanywa na taasisi hizo mbili kwa pamoja.

Kambi hiyo iliyofanyika kwa siku mbili hivi karibuni, ilihusisha jopo la wataalamu wa fani mbalimbali za udaktari waliotoa huduma za ushauri, vipimo, utambuzi wa magonjwa, pamoja na elimu ya afya kwa umma baada ya kupata idhini kutoka serikalini.

Katika kambi hiyo, jumla ya wagonjwa 182 walihudumiwa katika idara tofauti za kibingwa na zile za kawaida.

Idara ya macho (Optometrists) iliongoza kwa kuhudumia wagonjwa 43, ikifuatiwa na idara ya uchunguzi wa saratani iliyohudumia wanawake 36, huku daktari wa kawaida akihudumia watu 30.

Idara nyingine zilizotoa huduma ni pamoja na meno (wagonjwa 29), mfumo wa mkojo na uzazi kwa wanaume (wagonjwa 26), magonjwa ya wanawake (wagonjwa 10), pamoja na idara ya mifupa iliyohudumia wagonjwa 8.




Ripoti ya kambi hiyo imebainisha kuwa katika idara ya mfumo wa mkojo (Urology), matatizo yaliyoonekana zaidi ni pamoja na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), kutanuka kwa tezi dume (BPH), mawe kwenye figo, na changamoto za kushindwa kutoa mkojo.

Kwa upande wa uchunguzi wa saratani ya matiti, uliofanywa na Taasisi ya Shujaa kwa kushirikiana na Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, wanawake wote 36 waliofanyiwa vipimo walikutwa wakiwa salama bila dalili zozote za ugonjwa huo.

Aidha, changamoto nyingine za kiafya zilizojitokeza ni pamoja na matatizo ya kutoona vizuri na maambukizi ya macho, matatizo ya meno kama kuoza na maumivu ya fizi, pamoja na magonjwa ya mifupa kama maumivu ya mgongo na viungo.

Katika kliniki ya kawaida, magonjwa ya malaria, shinikizo la juu la damu, na maambukizi ya njia ya hewa yalikuwa miongoni mwa malalamiko makuu ya wagonjwa waliofika kambini hapo.

No comments