WAZIRI SANGU AZINDUA BARAZA JIPYA LA WAFANYAKAZI OWM-KAM, ATANGAZA VIPAUMBELE VYA KIMKAKATI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, amezindua rasmi Baraza jipya la Wafanyakazi la ofisi hiyo, huku akitoa maelekezo mazito kuhusu uzingatiaji wa uadilifu na uwajibikaji ili kuongeza ufanisi serikalini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma, Machi 25, 2026, Mhe. Sangu amesisitiza kuwa Baraza hilo ni chombo muhimu cha kukuza mahusiano mema mahali pa kazi na kuimarisha ustawi wa watumishi.
Mwelekeo wa Kimkakati na Vipaumbele vya Wizara
Katika hotuba yake Waziri Sangu ameanika vipaumbele nane (8) ambavyo Baraza hilo linapaswa kuvisimamia kwa ukaribu ili kuleta mapinduzi katika sekta ya kazi na ajira nchini.
.Usimamizi wa Sheria: Kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa sheria za kazi nchini.
.Mapitio ya Sera: Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili iendane na mazingira ya sasa.
.Ukuzaji Ujuzi: Kuratibu na kuimarisha mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa nguvu kazi ya taifa.
.Ajira za Nje: Kuratibu na kusimamia fursa za ajira kwa Watanzania nje ya nchi.
.Majadiliano ya Utatu: Kuratibu majadiliano kati ya Serikali, Waajiri, na Wafanyakazi.
.Marekebisho ya Sheria: Kupitia sheria za kazi na hifadhi ya jamii ili kuleta tija.
.Miongozo ya Mahusiano: Kuandaa miongozo itakayoboresha mahusiano kazini.
.Maandalizi ya Mei Mosi: Kuratibu na kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Pongezi kwa Taasisi za Kisekta
Waziri huyo hakusita kuzimwagia sifa taasisi tano (5) zilizo chini ya ofisi yake kwa utendaji uliotukuka. Taasisi hizo ni pamoja na WCF, PSSSF, NSSF, OSHA, na CMA, akibainisha kuwa zimekuwa mstari wa mbele kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli za Viongozi na Wadau
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo na Mwenyekiti wa Baraza, Mary Maganga, amemhakikishia Waziri kuwa atasimamia kwa karibu utekelezaji wa maagizo hayo ili kuhakikisha kunakuwepo na mazingira rafiki ya kazi yanayochochea tija.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Cde. Rugemalira Rutatina, amelipongeza Baraza hilo jipya na kuikumbusha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu umuhimu wa kuwa kioo katika kuzalisha wafanyakazi bora, hususan kwa nafasi yao ya uratibu wa sikukuu ya Mei Mosi.
Chimbuko la Baraza Jipya
Kuundwa upya kwa Baraza hili kumetokana na mabadiliko ya kimuundo ya Serikali yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo Novemba 17, 2025. Mabadiliko hayo yaliipa Ofisi ya Waziri Mkuu majukumu mapya ya kusimamia Kazi, Ajira na Mahusiano, hatua iliyolazimu kuanzishwa kwa chombo hiki cha majadiliano.
Katika kikao hicho cha kwanza, wajumbe pia wamepata fursa ya kupokea mada maalum kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii na fidia (PSSSF na WCF) ili kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na mafao.

Post a Comment