WASICHANA WA TANZANIA SI WATAZAMAJI TENA KWENYE STEM
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa tamko zito duniani ikisisitiza kuwa wakati wa wanawake na wasichana kuwa watazamaji kwenye nyanja za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) umekwisha, huku ikitangaza mageuzi makubwa ya kisera kuelekea Dira ya 2050.
Akizungumza kwa kujiamini jijini New York, Marekani, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Anna Athanas, amesema kuwa kuondoa vikwazo vinavyowazuia wasichana kushiriki kikamilifu katika fani hizo si ombi, bali ni hitaji la lazima kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Katika mjadala maalum ulioandaliwa na Chama cha Wahandisi Tanzania (Tawi la Wanawake) pembezoni mwa mkutano wa 70 wa Hali ya Wanawake Duniani, Mhe. Athanas amebainisha kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi wa viwanda, ubunifu na mifumo ya kisasa ya afya unategemea nguvu ya wasichana katika sayansi.
Licha ya takwimu za kimataifa kuonyesha wanawake ni asilimia 33 tu ya watafiti duniani, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za makusudi kupitia:Sera ya Jinsia 2023 kwa kuimarisha uwezeshaji kiuchumi na ushiriki wa wanawake katika sekta zisizo za jadi (Science & Engineering);Sera ya Elimu na Mafunzo 2023 kwa kuboresha mitaala na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ujifunzaji kuanzia ngazi ya sekondari na Dira ya 2050: Inayoweka Sayansi na Ubunifu kama kitovu cha ujenzi wa uchumi wa maarifa.
Waziri Athanas amekemea vikwazo vya kimfumo ambavyo vimekuwa vikiwakwamisha wasichana kuchagua masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati. Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa klabu za sayansi mashuleni na programu za uelekezi (mentorship) zinapewa kipaumbele ili kuwafikia maelfu ya wasichana nchi nzima.
"Tunapowawezesha wasichana katika sayansi na teknolojia, hatuwasaidii wao pekee, bali tunawezesha maendeleo ya taifa zima. Kuondoa vikwazo hivi ni kufungua milango ya suluhisho za kiubunifu zitakazonufaisha jamii yote ya Watanzania," alisisitiza Mhe. Athanas.
Hatua hizi zinathibitisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa dhati kugeuza Tanzania kuwa kitovu cha teknolojia barani Afrika, huku ikishirikiana na sekta binafsi na washirika wa maendeleo duniani kote ili kujenga mazingira jumuishi.

Post a Comment