e-Utatuzi mkombozi kasi kukabili migogoro ya kazi Tanzania





Safari ya mageuzi ya kidijitali nchini Tanzania imepiga hatua nyingine kubwa kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri ujulikanao kama e-Utatuzi. 

Katika kipindi cha siku 40 tu tangu kuanza mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri ujulikanao kama e-Utatuzi, katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA),mfumo huo umeweza kusajili migogoro 663, idadi ambayo ni kubwa kulinganisha na awali ambapo malalamiko hayakuzidi 300 kwa mwaka mzima.

Aidha mafanikio ya mfumo huu yanajidhihirisha katika ufanisi wa utatuzi wa mashauri, ambapo asilimia 40 ya migogoro iliyosajiliwa imeshafanyiwa maamuzi au kuhitimishwa. 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla, wakati anawaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii  ilipofanya ziara makao makuu ya Tume hiyo jijini Dar es salaam Machi 18,2026.

Mfumo huu, uliozinduliwa Januari mwaka huu  umewezeshwa na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mkombozi kwa wafanyakazi na waajiri kwa kuondoa vikwazo vya kijiografia na urasimu uliokuwa ukichelewesha upatikanaji wa haki kwa miaka mingi. 

Mpula alibainisha kuwa e-Utatuzi imesaidia kupunguza mlundikano wa kesi kutoka 20,000 hadi kufikia 7,000 pekee. Muhimu zaidi, mfumo umepunguza mianya ya rushwa kwa kuondoa "mtu wa kati," kwani mashine huchakata na kugawa mashauri kwa wasuluhishi kulingana na wingi wa kazi walizonazo (workload), jambo linaloongeza uwazi na imani kwa wananchi.

Aidha alisema kwamba kunaushirikiano wa kimfumo (Integration) ambao ni  uti wa mgongo wa mradi huu namba 5505, ambapo e-Utatuzi imeunganishwa na mifumo ya RITA, NIDA, Ofisi ya Kamishna wa Kazi,e-PERMIT na Mahakama Kuu kwa ajili ya kubadilishana taarifa. 

Alisema mkwamba hatua hiyo inahakikisha kuwa taarifa za walalamikaji na walalamikiwa zinahakikiwa kwa haraka, huku ikirahisisha ufuatiliaji wa mikataba ya kazi. Kupitia mfumo huo wadau wanaokoa muda na gharama za usafiri ambazo hapo awali zilikuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyakazi wa kipato cha chini.

Pamoja na mafanikio haya, ripoti ya CMA inataja maeneo matatu yanayoongoza kwa migogoro ya kazi nchini: kuachishwa kazi kinyume na taratibu, kuvunjiwa mikataba, na madai ya malimbikizo ya mishahara pamoja na posho. Hata hivyo ilibainishwa na wabunge kwamba pamoja na mafanikio hayo bado kuna pengo kubwa la uelewa wa sheria za kazi miongoni mwa waajiri na wafanyakazi, jambo linalopelekea malalamiko mengi kufika mbele ya wasuluhishi badala ya kumalizika katika ngazi ya mahali pa kazi.

Kisekta, takwimu zinaonesha kuwa sekta ya ujenzi, ulinzi binafsi, na mahoteli ndizo zinazoongoza kwa kuwa na migogoro mingi ya kikazi. Sekta hizi mara nyingi hukabiliwa na changamoto za mikataba ya muda mfupi, mazingira magumu ya kazi, na wakati mwingine kutoheshimiwa kwa viwango vya kima cha chini cha mshahara. 

Hali hii imeifanya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuitaka serikali kuongeza nguvu katika ukaguzi na elimu katika sekta hizi nyeti.

Ili kuendelea kukabiliana na migogoro, serikali imeongeza ikama ya watumishi wa Tume ambapo sasa watafikia 200 kutoka idadi ya mwanzo ya wafanyakazi 81.

Serikali, kupitia Naibu Waziri  Ofisi ya waziri Mkuu Kazi ajira na Mahusiano Rahma Riyadh Kisuo imesema kwamba itaendelea na kampeni yake ya "kutatua migogoro" na kuingia kwenye "kuzuia migogoro" (prevention). 

Aidha, serikali ikijibu hoja za wabunge katika mazungumzo imesisitiza kuwa ujenzi wa mfumo huu uliofanywa na wataalamu wazalendo (e-GA) umezingatia sheria zote za faragha na usalama wa data ili kulinda taarifa za watumiaji.

Wabunge, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Hawa Mchafu wameishauri serikali kuhakikisha bajeti iliyoombwa na CMA inatolewa kwa asilimia mia moja ili kukamilisha programu za mwaka wa fedha 2025/2026. 

Pia, wameitaka serikali kuhakikisha kuwa mfumo unalindwa kwa kuwajengea uwezo watumishi wa CMA kupitia mafunzo ya ndani na nje ya nchi ili kukabiliana na changamoto za usalama wa mitandao (cybersecurity) na uhalifu wa kidijitali (hacking), jambo ambalo ni muhimu katika kulinda uendelevu wa mfumo huo.

 e-Utatuzi ni kielelezo cha namna teknolojia inavyoweza kuchochea uchumi kwa kuruhusu watu kutumia muda mwingi katika uzalishaji badala ya kusubiri milolongo ya kesi mahakamani. 

Jitihada za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kugharamia mradi huu, zimeweka msingi imara wa haki na usawa mahali pa kazi, huku zikiimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania kupitia usuluhishi wa kisasa na wenye tija.


No comments