Utalii injini inayochochea ajira na kuimarisha huduma za kijamii





Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka wazi kuwa nguvu ya sekta ya utalii nchini haipaswi kupimwa kwa wingi wa fedha zinazoingia kwenye mfuko wa serikali pekee, bali kwa namna inavyogusa maisha ya mwananchi mmoja mmoja kupitia mnyororo mpana wa thamani.

Akizungumza jijini Arusha kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha Tuzo za Kitaifa za Uhifadhi na Mazingira (The Serengeti Awards), Dkt. Mwigulu amesema uhifadhi ni injini inayochochea ajira na kuimarisha huduma za kijamii.

"Faida ya utalii haiishii kwenye mapato pekee. Inajumuisha manufaa mapana yanayoifikia jamii pamoja na mnyororo mzima wa thamani unaotokana na uhifadhi. Serikali itaendelea kuhakikisha faida hizi zinamfikia mwananchi wa kawaida," alisema Dkt. Mwigulu.

Katika uchambuzi wake, Waziri Mkuu alibainisha kuwa sekta ya utalii inategemea mazingira yaliyohifadhiwa vyema. Alisisitiza kuwa bila jitihada za makusudi za kutunza rasilimali asilia, uchumi wa maeneo yanayozunguka hifadhi utatetereka.

Sekta hiyo imetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara ndogo kama za mama lishe, wauza vinyago, na wasafirishaji .Aidha mapato ya utalii yanasaidia ujenzi wa zahanati na shule katika vijiji vya jirani na hifadhi huku maelfu ya vijana wakiwa wameajiriwa kama waongoza watalii, madereva, na wahudumu wa hoteli.

Sauti za Wananchi

Wakizungumza nje ya ukumbi wa tuzo hizo, baadhi ya wakazi wa Arusha na wadau wa utalii wamepongeza kauli hiyo ya serikali, wakisema inatoa picha ya uhalisia wa maisha yao ya kila siku.

Bwana Juma Bakari, ambaye ni dereva wa magari ya watalii kwa zaidi ya miaka kumi, alisema: "Ni kweli kabisa, watalii wasipokuja, siyo serikali tu inayokosa kodi, bali hata sisi mtaani hatuna kitu. Akija mtalii mmoja, mimi napata mshahara, mama ntilie anauza chakula, na kijana wa kuosha gari anapata riziki yake."

Naye Bi. Rehema Mollel, mfanyabiashara wa vinyago na ushanga, aliongeza: "Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutangaza utalii (Royal Tour). Sisi tunaoishi karibu na hifadhi tunaona faida moja kwa moja, kwani soko letu linategemea wageni hawa."

Dkt. Mwigulu ambaye alihitimisha kwa kutoa rai kwa wadau wa mazingira kuendelea kushirikiana na serikali amesisitiza kuwa tuzo hizo za Serengeti  ni kielelezo cha kutambua mchango wa wale wanaopambana kulinda urithi wa nchi kwa ajili ya vizazi vijavyo na uchumi wa sasa.

No comments