DIPLOMASIA YA NISHATI: Tanzania Kupata Msaada wa Kiufundi wa AfDB Kugeuza Ahadi Kuwa Vitendo
Tanzania ni miongoni mwa nchi 13 barani Afrika zitakazonufaika na mpango mpya wa nishati baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuidhinisha mradi wa msaada wa kiufundi wa thamani ya dola za Kimarekani milioni 3.9.
Mradi huu wa miaka miwili unalenga kusaidia utekelezaji wa mipango ya nishati kwa vitendo kupitia mpango wa Mission 300, ambao ni ushirikiano kati ya AfDB na Benki ya Dunia wenye lengo la kuunganishia umeme watu milioni mia tatu barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Mikataba ya Nishati ambayo sasa inakwenda kutekelezwa ni mipango ya kitaifa ambapo serikali huainisha namna zitakavyopanua upatikanaji wa umeme, kuimarisha sekta za nishati, na kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, mataifa kadhaa ya Afrika yamezindua mikataba hii ikiungwa mkono na dhamira thabiti ya kisiasa ili kuhakikisha nishati safi na ya uhakika inamfikia mwananchi wa kawaida kuanzia mijini hadi vijijini.
Mradi huu mpya unaojulikana kama AESTAP Mission 300 Awamu ya Pili, utatoa msaada wa moja kwa moja wa kiufundi kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Chad, Gabon, Mauritania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria, Madagascar, Ethiopia, Malawi, Lesotho, na Namibia. Ndani ya kipindi cha miezi 24 ijayo, nchi hizi zitawezeshwa kuhama rasmi kutoka kwenye mipango iliyoandikwa kwenye nyaraka na kuanza kuunganisha umeme kwenye nyumba za kuishi, shule, hospitali, na maeneo mbalimbali ya biashara.
Katika utekelezaji wake wa kivitendo, mradi huu utazisaidia serikali husika kuboresha kanuni za umeme, mipango ya muda mrefu, na mifumo ya bei za nishati ili kuruhusu uwekezaji wa sekta binafsi kusonga mbele kwa kasi zaidi. Vilevile, utasaidia kuimarisha mashirika ya umeme ili yaweze kutoa nishati yenye tija na kupunguza upotevu wa nishati wakati wa usambazaji, huku washauri wataalamu wakiwekwa ndani ya vitengo vya kitaifa vya ufuatiliaji ili kusaidia serikali kuratibu mageuzi hayo.
Mkurugenzi wa Masuala ya Kifedha ya Nishati, Sera na Kanuni wa AfDB, Wale Shonibare, amebainisha kuwa nchi zimefanya ahadi kubwa na sasa benki hiyo inazisaidia kutekeleza ahadi hizo ili kaya, wajasiriamali, na jamii kwa ujumla zipate huduma ya umeme.
Hata hivyo hatua hii inafuatia mafanikio ya Awamu ya Kwanza ya mradi huo iliyoidhinishwa Desemba 2025, ambayo ilijikita katika kuunda na kuimarisha timu za utekelezaji pamoja na kuandaa zana za kisasa za ufuatiliaji wa maendeleo ya nishati.
Awamu hii ya pili itajenga juu ya msingi huo kwa kutoa msaada wa kiufundi unaohitajika kutekeleza mageuzi yaliyopangwa kwa ushirikiano na washirika wengine wa Mission 300 ikiwemo Benki ya Dunia na mashirika ya kimataifa.
Lengo kuu ni kuhakikisha juhudi hizi za pamoja zinaleta tija na mabadiliko ya kweli katika maisha ya waafrika, huku Tanzania ikitajwa kuwa mshirika muhimu katika kufanikisha mapinduzi haya ya nishati kuelekea uchumi wa viwanda na ustawi wa jamii.

Post a Comment