Barabara za Mwendokasi Kufungua Ukurasa Mpya wa Ajira na Mapinduzi ya Kiuchumi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua ya kijasiri kuelekea mabadiliko makubwa ya miundombinu baada ya kuzindua Mpango Kabambe wa Ujenzi wa Barabara za Mwendokasi nchini unaojulikana kama Tanzania Expressway Master Plan.
Uamuzi huu wa kimkakati, unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Ushirikiano la Kimataifa la Korea (KOICA), unalenga kutibu kero ya muda mrefu ya msongamano wa magari huku ukiandaa njia ya kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Hatua hii ya serikali imekuja wakati muafaka ambapo kukua kwa uchumi wa nchi kunahitaji mifumo ya usafirishaji inayokwenda na kasi ya kidijitali. Kwa kuwekeza kwenye barabara hizi kubwa na za kisasa, serikali inalenga si tu kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, bali pia kupunguza gharama za kufanya biashara ambazo mara nyingi huathiriwa na ucheleweshaji barabarani.
Huu ni mkakati unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, jambo litakaloongeza mzunguko wa fedha kuanzia ngazi ya kitaifa hadi kwa mwananchi mmoja mmoja.
Katika kilele cha uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ameweka msisitizo mkubwa juu ya ustawi wa vijana ambao ndio nguvu kazi kuu ya taifa.
Waziri Ulega amebainisha kuwa mradi huu ni darasa tosha kwa wataalamu wazawa, hususan wahandisi vijana, ambapo amewataka kujikita kikamilifu katika kujifunza teknolojia mpya za ubunifu na usimamizi wa miradi mikubwa.
Lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa kupitia mradi huu, nchi inajenga jeshi la wataalamu wa ndani watakaoweza kuendesha miradi mingine ya kimkakati bila kutegemea nguvu ya nje katika siku za usoni.
Kwa upande wa maendeleo ya kijamii, mpango huu unaashiria neema kwa vijana wanaotafuta fursa za ajira na ujasiriamali. Ujenzi wa barabara hizi utachochea kuanzishwa kwa miji mipya na maeneo ya kibiashara pembezoni mwa barabara hizo, jambo litakalotoa fursa kwa vijana wabunifu kuanzisha miradi ya usafirishaji, karakana za kisasa, na huduma nyinginezo.
Hii inatajwa kuwa ni njia mojawapo ya kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa kuwapa vijana jukwaa la kuonesha uwezo wao katika ujenzi wa taifa.
Ushirikiano huu wa kihistoria umetiwa nguvu na ruzuku ya dola za Kimarekani milioni tano kutoka serikali ya Korea, fedha ambazo ni matokeo ya mkataba wa makubaliano uliosainiwa Agosti 2025.
Meneja wa Miradi ya Ubia kutoka TANROADS, Mhandisi Elibariki Mkumbo, ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huu kwa mwaka huu unajenga msingi imara wa diplomasia ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, wadau wa maendeleo wameshauri kuwepo kwa muunganiko wa karibu kati ya sekta ya ujenzi, nishati, na makazi ili kuhakikisha kuwa barabara hizi zinachochea maendeleo ya jumla bila kuleta migongano ya miundombinu mingine kama reli na viwanja vya ndege.

Post a Comment