Uingereza Yaendelea Kutikisa Soko la Usajili Duniani



Vilabu vya soka nchini Uingereza vimeendelea kutawala soko la usajili duniani kwa kutumia kiasi cha dola milioni 363 katika dirisha la mwezi Januari mwaka huu wa 2026. 

Hata hivyo kiasi hicho ni kidogo ikilinganishwa na dola milioni 623 walizotumia kipindi kama hiki mwaka jana, jambo linaloashiria vilabu hivyo kuanza kuwa na nidhamu zaidi ya kifedha.

Kwa mujibu wa ripoti ya FIFA ya usajili wa kimataifa, mwezi Januari umeweka rekodi ya kihistoria kwa kuwa na zaidi ya uhamisho wa wachezaji 5,900 duniani kote. Hili ni ongezeko la asilimia 3 ya idadi ya wachezaji waliohama, licha ya kuwa jumla ya fedha zilizotumika duniani kote zilishuka kwa asilimia 18 hadi kufikia dola bilioni 1.9.

Nyuma ya Uingereza, vilabu vya Italia vilishika nafasi ya pili kwa kutumia dola milioni 283, huku Brazil ikishangaza kwa kushika nafasi ya tatu kwa kutumia dola milioni 180. Moja ya usajili mkubwa ulioangaziwa ni wa mchezaji wa kimataifa wa Brazil, Lucas Paquetá, aliyeondoka West Ham ya Uingereza na kujiunga na Flamengo kwa dau la takriban dola milioni 49.

Kwenye soka la wanawake  matumizi yamepaa kwa asilimia 85 na kufikia dola milioni 10. Katika sekta hiyo pia, Uingereza imeendelea kuonyesha ubabe wake kwa kuchangia zaidi ya nusu ya fedha hizo, ikitumia zaidi ya dola milioni 5 kusajili nyota wapya.

No comments