JINSI SERIKALI INAVYOJIBU KILIO CHA AJIRA KWA VIJANA NCHINI TANZANIA
Katika hatua inayotajwa kama "mkombozi wa vijana," Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kutekeleza mkakati kabambe wa kupunguza msongamano wa wasaka ajira nchini kwa kufungua milango ya fursa za kimataifa na kuimarisha mazingira ya ujasiriamali ndani ya nchi.
Hatua ya hivi karibuni ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, kusaini mikataba mitano ya ajira nje ya nchi, ni uthibitisho tosha kuwa kilio cha vijana sasa kimepata majibu ya vitendo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kipindi cha ‘Imbeju - Bongo Fursa’ na Jarida la Mapitio ya Vijana, Waziri wa Nchi, Mhe. Deus Sangu, amesema kuwa serikali imesikia kilio cha vijana na sasa inachukua hatua za kidiplomasia kupanua soko la nguvu kazi. Waziri Sangu amebainisha kuwa, mbali na mikataba hiyo mitano iliyokamilika, kwa sasa serikali iko katika hatua za mwisho za majadiliano ya mikataba mingine 16 ya ajira.
Hatua hii ni jibu la moja kwa moja kwa changamoto ya uhaba wa ajira ndani ya nchi, ambapo serikali imeamua kutumia uhusiano wake mzuri wa kimataifa kama daraja la kuwavusha vijana. Waziri Sangu alisisitiza kuwa ziara yake hivi karibuni katika nchi za Falme za Kiarabu imedhihirisha kuwa mataifa mengi yana imani na nidhamu pamoja na ujuzi wa vijana wa Kitanzania, jambo linalofungua fursa nyingi zaidi.
Sambamba na ajira za nje, serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazingira ya ujasiriamali ndani ya nchi. Kupitia Baraza la Taifa la Biashara na Maendeleo (NEDC), kumezinduliwa majukwaa maalum ya kuwaibua wabunifu na wajasiriamali wadogo. Mkurugenzi wa NEDC, Jesse Madauda, amefafanua kuwa lengo la juhudi hizo ni kuwakutanisha vijana wabunifu na wawekezaji ili waweze kupata mitaji na miongozo itakayowasaidia kukuza biashara zao.
Kwa upande wao, vijana wajasiriamali wameipongeza serikali kwa kuonesha nia ya dhati ya kuwashika mkono. Elizabeth Consoli, mmoja wa wajasiriamali waliojitokeza, amesema kuwa uwepo wa serikali karibu na wavumbuzi unawapa moyo na uhakika wa kuvuka kutoka hatua ya awali kwenda katika biashara kubwa zenye tija kwa taifa.
Utekelezaji wa mikataba hii na uzinduzi wa majukwaa ya fursa ni kielelezo tosha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inatenga nafasi ya kipekee kwa vijana. Kilio cha muda mrefu cha "tumesoma lakini hatuna kazi" sasa kinageuzwa kuwa "tuna ujuzi, tunatafuta fursa" huku serikali ikijenga mazingira rafiki ya kuunganisha vijana hao na fursa husika.

Post a Comment