TAFFA 2026: MSIGWA AHIMIZA FILAMU ZA MABILIONI, ‘MY SON’ YATAWALA JUKWAA
Serikali imetoa wito mzito kwa wasanii nchini kuachana na utengenezaji wa filamu za mazoea na badala yake wajikite katika ubora utakaowawezesha kushindana kimataifa na kuliingizia taifa fedha za kigeni (Dola).
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, wakati wa kilele cha Tuzo za Filamu Tanzania (TAFFA 2026) zilizofanyika usiku wa kuamkia juzi katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini hapa.
Msigwa alisema kuwa tasnia ya filamu ni biashara ya mabilioni ya fedha iwapo itaendeshwa kwa weledi na kufuata misingi ya kitaalamu. Alisisitiza kuwa serikali imeshajipanga kuweka mazingira wezesha, ikiwemo mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kujenga studio ya kisasa yenye thamani ya Shilingi bilioni 150.
“Tukisimamia ubora na filamu zetu zikafikia viwango vya kimataifa, tutapata Dola za Marekani kwani watengeneza filamu duniani ni mabilionea. Suala hapa ni ubora na si kufanya kazi kwa mazoea ya ‘heya heya’. Bila ubora, utaishia kupata shilingi milioni mbili tu badala ya mabilioni,” alisema Msigwa.
'My Son' Yazoa Tuzo Sita
Katika usiku huo uliotawaliwa na shamrashamra, filamu ya ‘My Son’ iliibuka mshindi wa kishindo kwa kunyakua jumla ya tuzo sita. Filamu hiyo ilishinda katika vipengele vya Filamu Bora Ndefu, Muongozaji Bora (Ramar King), Muigizaji Bora wa Kiume (Isarito Mwakalindile), Sauti Bora, Haiba (Production Design), na Picha (Cinematography).
Akizungumzia mafanikio hayo, Muigizaji na Mtayarishaji Isarito Mwakalindile, alisema siri ya ushindi wao ni muda na maandalizi ya kina.
“Kutengeneza filamu bora inahitaji muda, filamu sio kama kutengeneza maudhui (content) za mtandaoni. Filamu yetu ilichukua miezi mitano na ilitumia bajeti kubwa. Tunaamini kazi kubwa tuliyoifanya ndiyo iliyoonekana na kupigiwa chapuo la ubora,” alisema Isarito.
Mafanikio ya TAFFA 2026
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Studio 19 (waandaaji wenza wa tuzo hizo), Brian Paul, alisema tamasha la mwaka huu limekuwa la kihistoria na lenye tija kubwa kwa tasnia.
Alibainisha kuwa ukumbi wa Super Dome ulikuwa na watazamaji zaidi ya 1,000 hadi majira ya saa tisa alfajiri, jambo linaloonyesha kukua kwa hamasa ya filamu nchini.
“Tamasha sasa limeanza kuwa la kimataifa kwani tumepokea kazi kutoka nchi jirani. Huu ni wakati wa watengeneza sinema kuangalia ubora zaidi ili kazi zao ziweze kuvuka mipaka,” alisema Paul.
Washindi Wengine na Tuzo za Heshima
Katika usiku huo, tasnia iliwaenzi wakongwe ambapo mwigizaji Abdallah Mkumbillah (Muhogo Mchungu) na Profesa Amandina Lihamba walitunukiwa Tuzo za Heshima kwa mchango wao mkubwa katika uigizaji na sanaa nchini.
Orodha ya washindi wengine ni pamoja na:
Muigizaji Bora wa Kike: Maryam Ismail.
Tamthiliya: Salim Ahmed (Gabo Zigamba) na Shamira Ndwangila (Bistar).
Chipukizi Bora: Mwinyihamisi Bakari (Rionegro) na Elizabeth Chijumba (Nikita).
Mwongozaji Bora (Kike): Cece Mlay.
Chaguo la Watazamaji: Shamila Ndwangila (Bistar) na Rashid Ramadhan (Baraka Tatu).
Filamu Bora Fupi: Unasemaje.
Mavazi Bora: Baraluko.
Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk. Gervas Kasiga, alihitimisha kwa kuwasihi wasanii kutochoka kujiboresha. "Mwisho wa safari moja ya tuzo ni mwanzo wa maandalizi ya safari nyingine. Tuendelee kushirikiana kuifanya TAFFA kuwa kioo cha ubora wetu," alisema.



Post a Comment