DIPLOMASIA YA DKT. SAMIA YAZIDI KUING'ARISHA TANZANIA KIMATAIFA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa kupitia mfululizo wa mazungumzo ya kimkakati yaliyofanyika kando ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia. 

Hatua hiyo ya Rais Samia kupanua wigo wa diplomasia ya kiuchumi imetafsiriwa kama pigo kwa wale wasioitakia mema Tanzania. Kwa sasa Tanzania inazidi kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa viongozi wa mataifa mbalimbali barani Afrika kutokana na ushawishi wake unaozidi kukua siku hadi siku.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni kuimarika kwa mashirikiano ya kiuchumi Rais Samia alifanya mazungumzo na Rais wa Angola João Lourenço ambapo kiongozi huyo amekubali kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania na kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba mwaka 2026. 

Makubaliano hayo yanatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji katika sekta za nishati madini na viwanda huku viongozi hao wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya kihistoria kwa manufaa ya ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.

Vilevile Rais Samia alikutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Dkt. Abiy Ahmed Ali ambapo walijadili kuimarisha biashara na ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga na usimamizi wa rasilimali za maji. 

Mazungumzo hayo pia yaligusia mwelekeo wa ukuaji wa uchumi ambapo Tanzania inatarajia kufikia ukuaji wa asilimia 6.5 ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha maisha ya wananchi wake kupitia mipango madhubuti ya kiuchumi inayopata sifa ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Mafanikio hayo ya kidiplomasia yalihitimishwa kwa mazungumzo kati ya Rais Samia na Rais wa Comoro Azali Assoumani ambaye ametoa shukrani za dhati kwa mchango wa Tanzania katika kuimarisha huduma za afya na usalama nchini kwake. 

Rais Assoumani ameonesha nia ya kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania ikiwa ni ishara ya kutambua nafasi ya Tanzania kama muhimili wa amani na maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika hali inayozidi kuwadhalilisha wakosoaji wa uongozi wa Rais Samia wanaoshuhudia nchi hiyo ikipaa kimataifa kuelekea Dira ya Mwaka 2050.

No comments