Rotimi: Mimi na Vanessa Hatuachani Kamwe



Tetesi za kuachana kwa wapendanao maarufu, Vanessa Mdee na mumewe, mwigizaji na mwanamuziki Rotimi, zimezimwa rasmi baada ya wawili hao kuonekana pamoja na kuweka mambo hadharani.

Hivi karibuni, mitandao ya kijamii ilichafuka kwa uvumi kuwa penzi la wawili hao liko shakani, hasa baada ya kupunguza kasi ya kuposti maudhui wakiwa pamoja kama walivyozoeleka. Hali hiyo ilichochewa zaidi na picha za Rotimi akiwa kwenye mchezo wa mpira wa kikapu akiwa na mwanamke mwingine, jambo lililoibua maswali mengi miongoni mwa mashabiki.

"Usituchezee," Mashabiki wa Afrika Mashariki Wamtolea Uvivu Rotimi

Mashabiki wa Vanessa, hasa kutoka nchini Tanzania na Kenya, walivamia kurasa za mastaa hao wakionekana kuwa tayari "kumuwashia moto" Rotimi ikiwa tetesi hizo zingekuwa za kweli. Baadhi ya maoni yalisomeka:

Waruguru Wa Kiai: "Mwambie mumeo asijaribu kuichezea Afrika Mashariki mwaka huu wala mwingine wowote."

Wardah Yongo: "Kama Wakenya, mumeo anatujaribu sana uvumilivu wetu. Mkumbushe kuwa hatuchezi na wewe."

Thy: "Mkumbushe mumeo kuwa unapendwa nyumbani (Afrika Mashariki), asijaribu mchezo wowote."

Jibu la Rotimi: "Ni Mke Wangu wa Pekee"

Ili kukata mzizi wa fitina, Rotimi alipakia video fupi akiwa na mke wake na kueleza kuwa walikuwa kimya kwa sababu ya maandalizi ya albamu mpya. Katika video hiyo, Rotimi alitumia lugha ya Kiswahili kutoa msisitizo kwa mashabiki wa nyumbani kwa Vanessa.

"Mke wangu amewasili mjini, sasa ni muda wa kazi ya albamu. Watanzania, sisi hatuachani kamwe. Huyu ndiye mke wangu wa pekee," alisema Rotimi.

Safari ya Penzi Lao

Vanessa Mdee na Rotimi walikutana mwaka 2019 kwenye tamasha la Essence kule New Orleans, Marekani. Vanessa amewahi kukiri kuwa alijua Rotimi atakuwa mume wake ndani ya siku chache tu tangu wakutane. Baada ya mahusiano ya mbali kwa muda mfupi, Vanessa alihamia Marekani na kutangaza kuachana na kile alichokiita "kiwanda cha muziki chenye sumu."

Wawili hao walifunga ndoa mwaka 2021 na sasa wamejaliwa watoto wawili, huku wakiendelea kuwa mfano wa kuigwa wa "Couple Goals" kwenye mitandao ya kijamii.

No comments