RAIS SAMIA NA UAE ZAKUBALIANA KUPANUA WIGO WA BIASHARA NA UTALII




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo ya pande mbili na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa UAE, Mtukufu Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, mjini Dubai tarehe 04 Februari 2026. 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa World Government Summit, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha Mikataba ya Ushirikiano wa Biashara (CEPA) na ile ya Uwekezaji (BIT) ili kuimarisha mazingira ya biashara baina ya nchi hizo mbili.

Mbali na mikataba hiyo, viongozi hao wamejadili uwezekano wa kuanzishwa kwa safari mpya za anga za Shirika la Ndege la Emirates, hususan njia ya Kilimanjaro kuelekea Zanzibar, hatua inayolenga kukuza sekta ya utalii na biashara. 

Kwa upande wake, Sheikh Mohammed ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika miradi ya maendeleo kwa manufaa ya kiuchumi ya pande zote mbili.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewasilisha uzoefu wa Tanzania katika kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisheria mbele ya Jukwaa la Serikali Duniani. 

Amebainisha kuwa Tanzania imeweka mkazo katika ujenzi wa miundombinu ya kimkakati kama reli ya kisasa (SGR), barabara, na bandari ili kuwa kitovu cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 Uhusiano huu unakuja wakati thamani ya biashara kati ya Tanzania na Dubai ikifikia dola bilioni 2.1 kwa mwaka 2024, jambo linaloifanya Tanzania kuwa mshirika wa nne kwa ukubwa wa biashara wa UAE barani Afrika.

No comments