Konde na Kajala: Penzi Limerudi, Pete Imekaa


Hatimaye kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa burudani nchini Tanzania kimejiri baada ya msanii Harmonize kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake, Frida Kajala Masanja. Tukio hilo la kusisimua limetokea mwezi mmoja tu baada ya wawili hao kuonekana hadharani wakibusiana ikiwa ni dalili za hao wawili kurudiana.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kajala ameweka wazi furaha yake kwa kushirikisha mfululizo wa picha zinazomuonyesha Harmonize akiomba ridhaa ya kumuoa, huku yeye akikiri kukubali kwa neno "Ndiyo". 



Katika picha hizo, Kajala alionekana mrembo akiwa amevaa gauni refu jeusi na nywele fupi zenye mawimbi, huku Harmonize akipendeza na shati la mistari na suruali ya rangi ya 'cream'. Moja ya picha zilizovuta hisia za wengi ni ile inayomwonyesha msanii huyo akimbeba Kajala mgongoni, huku wageni waalikwa waliokuwa wamevalia mavazi meupe wakishuhudia tukio hilo kwa mshangao na furaha.

Harmonize hakuishia hapo, kwani alimwagia sifa kedekede mpenzi wake huyo akimtaja kama zawadi kutoka kwa Mungu. Alieleza kuwa kila siku anayokaa na mwanamke huyo inamfundisha maana halisi ya upendo, heshima, na amani, akisisitiza kuwa amemchagua kuwa mke wa maisha yake leo, kesho, na milele. 



Hatua hii imekuja baada ya safari ndefu ya uhusiano wao iliyojaa milima na mabonde, ikiwemo kuachana kwao kwa kishindo mwaka 2022 licha ya Harmonize kutoa zawadi za thamani kama magari na vito.

Mashabiki na watu maarufu wamefurika katika mitandao ya kijamii kuwapongeza, wengi wakiamini kuwa huu ni uthibitisho wa mapenzi ya dhati yanayostahimili majaribu. 

Hivi karibuni, Kajala alizidi kuweka wazi ukaribu wao kwa kufichua kuwa Harmonize amekuwa naye kwa muda mrefu, hata kipindi anaanza muziki alimsaidia kumlipia ada binti yake, Paula, jambo ambalo lilionyesha kuwa urafiki wao una misingi imara. Tukio hili la kuvishana pete sasa linafungua ukurasa mpya wa safari yao kuelekea ndoa.



No comments