SALOME MAKAMBA AZIAMSHA TAASISI ZA FEDHA, KUSAIDIA VIJANA WABUNIFU NISHATI SAFI
Serikali imezitaka taasisi za fedha nchini kuelekeza nguvu na uwekezaji kwa wajasiriamali pamoja na wabunifu wa kidijitali waliojikita katika biashara ya nishati ili kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya taifa ya kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema wakati wa uzinduzi wa mradi wa nishati safi katika shule ya sekondari ya wasichana ya Bunge iliyopo mkoani Dodoma, ingawa matumizi ya nishati safi yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 23.2 mwaka 2025, bado kuna safari ndefu ya mafanikio kwani takribani asilimia 77 ya kaya bado zinatumia nishati isiyo safi.
Naibu Waziri amewasisitiza wasambazaji wa gesi ya mitungi kuongeza vituo vya usambazaji na ujazaji ili kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi wengi zaidi, huku akiwahamasisha wabunifu na vijana walioko vyuoni kufanya tafiti na kubuni teknolojia zitakazorahisisha usambaaji wa ajenda hiyo nchi nzima.
Mradi huo uliomalizika shuleni hapo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali linalozitaka taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ili kulinda afya za binadamu na kutunza mazingira, hatua inayokwenda kuokoa gharama kubwa kwani shule hiyo yenye wanafunzi 555 imekuwa ikitumia wastani wa shilingi milioni 10.5 kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya ununuzi wa kuni pekee.

Post a Comment