Infocus Studio yapania kuneemesha Watanzania kwa teknolojia ya Canon
Mkurugenzi Mtendaji wa Infocus Studio, Joshua Moshi, amesema kuwa lengo kuu la kampuni hiyo ni kuhakikisha maarifa, viwango na weledi wanaoutumia katika utengenezaji wa maudhui unawafikia na kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi.
Akizungumza katika ziara ya uongozi wa juu wa Canon Europe, Moshi amesisitiza kuwa amekuwa akitafuta njia ya kurudisha ujuzi huo kwa jamii ili manufaa ya kazi zao yaguse makampuni mengine tanzu na wabunifu wazawa nchini kote.
Ameongeza kuwa uwekezaji mkubwa wanaoufanya katika vifaa vya kisasa si suala la muonekano pekee, bali ni msingi wa kujenga ubora na uimara wa kazi zao kwa muda mrefu ili kuendana na kasi ya soko la kidunia.
![]() |
| Mkurugenzi Mtendaji wa Infocus Studio, Joshua Moshi, wa tatu kushoto, akiwa na ugeni wake. |
Ziara hiyo ya kikazi iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Canon Europe, Ozgur Kocademir, imekuja kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kutathmini hatua zilizofikiwa katika kuendeleza tasnia ya picha na video nchini.
Kocademir amevutiwa na ari ya Infocus Studio na kueleza kuwa ushirikiano huo ni wa pande mbili na una tija kubwa katika kuongeza uzoefu wa pamoja kwa mwaka huu wa 2026 na kuendelea. Pande zote mbili zimejadili kwa kina jinsi ya kuvuka mipaka ya uzalishaji maudhui Afrika Mashariki ili yaweze kufika barani kote na duniani kote kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Katika kuitikia mabadiliko ya teknolojia, Infocus Studio imewekeza katika ununuzi wa kamera mpya za kisasa za Canon C50 toleo la mwaka 2026, ambazo zina uwezo mkubwa wa kurekodi kwa ubora wa juu na kutumia teknolojia ya Akili Bandia (AI).
Uwekezaji huu unalenga kuongeza ushindani wa kampuni hiyo katika soko la ndani na kimataifa, huku ukiongeza ufanisi katika mazingira ya uzalishaji wa maudhui ya kisasa yanayohitaji ubora wa hali ya juu. Hatua hiyo inaashiria namna ushirikiano kati ya kampuni za ndani na viongozi wa teknolojia duniani unavyoweza kuchochea maendeleo katika tasnia ya ubunifu nchini.
Infocus Studio imekuwa mdau muhimu nchini Tanzania kwa kufanya kazi na taasisi kubwa zikiwemo Benki ya CRDB, Benki ya Dunia, Vodacom, pamoja na wizara mbalimbali za Serikali katika kurusha matukio mubashara na kutengeneza video.
Kampuni hiyo pia imejizolea sifa katika miradi mikubwa ya burudani barani Afrika ikiwemo tamasha la Castle Lite na kushiriki katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia wageni maarufu kama Braydon Bent.
Kwa sasa, Infocus na Canon wanajipanga kutekeleza mipango yao ya pamoja kwa lengo la kupanua wigo wa kazi zao na kuendelea kuwa kioo cha ubora wa maudhui ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.





Post a Comment