RAIS DKT. SAMIA ATOA MAELEKEZO MAZITO KWA VIONGOZI WAPYA, ASISITIZA KUFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi waliokula kiapo cha uadilifu Februari 9, Ikulu jijini Dar es Salaam kuhakikisha kuwa maendeleo ya Taifa yanaakisiwa na mabadiliko ya vitendo na uwajibikaji wa haraka. 

Rais amesisitiza kuwa uteuzi huo umelenga kuimarisha ufanisi wa Serikali ili kuendana na kasi ya mahitaji ya wananchi na kuhakikisha mipango ya nchi inatekelezwa kwa wakati.

Akizungumzia mwelekeo wa kiuchumi, Rais Dkt. Samia ameweka wazi kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ina matarajio makubwa ambapo sekta binafsi inatarajiwa kubeba mzigo mkubwa wa asilimia sabini katika kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka huo. 

Kutokana na umuhimu huo, ametoa agizo kali kwa viongozi wenye dhamana kuacha mara moja tabia ya kuchelewesha uwekezaji kwa sababu za kisheria na kiutawala, akisema kuwa ni lazima waondoe sheria zinazokwaza maendeleo na wafungue milango kwa wawekezaji.

Katika hatua nyingine, Rais ameelekeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuhakikisha inasimamia kikamilifu mikakati ya kufungua fursa za biashara na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kuchochea ajira na ukuaji wa uchumi.



 Vilevile, amewataka viongozi wa sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi kwa kuwa sekta hizo ndizo mhimili mkuu wa mapato kwa vijana.

Kuhusu sekta ya nishati na mazingira, Mheshimiwa Rais amebainisha lengo la Serikali la kuzalisha megawati elfu 8 za umeme ifikapo mwaka 2030 kupitia vyanzo mbalimbali vikiwemo maji, jua, gesi na mafuta ili kusaidia ukuaji wa viwanda. 

Aidha, amewahimiza viongozi kutumia fursa ya biashara ya hewa ukaa kuongeza mapato ya Taifa huku wakilinda mazingira.

Aidha amewakumbusha viongozi wa mikoa ya kimkakati ya Kagera na Mtwara kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha amani na utulivu vinatawala katika maeneo yao kwa ajili ya usalama wa nchi na uchumi.

No comments