Dkt. Nchimbi Awahimiza Viongozi wa Dini Kusimamia Maadili na Utunzaji wa Mazingira
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewataka viongozi wa dini nchini kuwa mstari wa mbele katika kuliombea Taifa, kusimamia maadili ya jamii, na kuwa mabalozi wa hifadhi ya mazingira.
Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo , tarehe 06 Februari 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusimikwa kwa Uongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Tano wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), iliyofanyika katika ukumbi wa Agape Life Church, Mbezi Jogoo.
Katika hotuba yake amewasihi viongozi hao kujenga Taifa linalomcha Mungu, lenye watu waaminifu, wanaopendana na wanaozingatia uzalendo, huku wakipiga vita ubinafsi na rushwa.
Aidha amesisitiza umuhimu wa kuliombea Taifa na kumuombea Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuongoza nchi kwa hekima, busara, na afya njema.
Kuhusu suala la hifadhi ya mazingira, Dkt. Nchimbi ametoa mwito wa kipekee kwa viongozi wa dini kuwafundisha waumini umuhimu wa kupanda miti na kulinda vyanzo vya maji ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.
Makamu wa Rais amebainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele katika mahusiano na taasisi za dini, ikiwemo kuunda Wizara maalum ya kusimamia uratibu huo.
"Serikali inatambua na kushukuru mchango mkubwa wa taasisi za dini katika sekta za kijamii kama elimu, afya, na malezi ya watoto," alisema Dkt. Nchimbi.
Katika kuonyesha ushirikiano huo kwa vitendo, alitangaza kuwa Rais Samia ametoa shilingi milioni 100 na eneo la hekari 12 mkoani Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Baraza hilo (CPCT).
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, alieleza kuwa serikali imekamilisha rasimu ya Mwongozo wa Kuratibu Mahusiano kati ya serikali na taasisi za dini, ambao utazinduliwa hivi karibuni ili kuimarisha zaidi ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa CPCT, Askofu Vernon Fernandes, ametoa shukrani kwa serikali kwa kuthamini nafasi ya viongozi wa dini na kuanzisha idara rasmi inayowanisha pande hizo mbili.




Post a Comment