DARASA LA UTAJIRI: BIDHAA TANO ZA VIJANA WA KITANZANIA KUPELEKA SOKO LA CHINA

 



Wakati Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ikitangaza rasmi sera ya ushuru sifuri kwa bidhaa kutoka Tanzania na nchi nyingine 52 za Afrika, kumeibuka swali la msingi: Je, kijana wa Kitanzania amejipangaje kunufaika na soko hili la watu bilioni 1.4?

Hatua hii ni fursa ya dhahabu inayohitaji mabadiliko ya fikra. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo biashara ilikuwa ni kuuza malighafi, soko la sasa linadai bidhaa zilizoongezwa thamani. Ni lazima vijana wetu wahamie kwenye viwanda vidogo na vya kati (SMEs) ili kutoa bidhaa zinazokidhi vigezo vya kimataifa.

"Huu si wakati wa kusubiri ajira za ofisini. China imetupa uwanja wa kucheza, na mpira uko miguuni mwetu. Vijana wanapaswa kuwa wabunifu na kuanza kutafuta msaada wa kutaalamikiwa (Export support) kutoka taasisi za Serikali kama TanTrade na SIDO," anasema mdau mmoja wa biashara za kimataifa.

Ni kweli kuwa badala ya kutumia mitandao ya kijamii kupaza sauti za kukata tamaa, huu ni wakati wa kutumia data na intaneti kutafuta mahitaji ya soko la China. Serikali imeshafanya kazi yake ya kidiplomasia na kufungua milango; sasa ni jukumu la mwananchi mzalendo, hasa kijana, kuingia na kufanya biashara yenye tija.

Hakika huu ni wakati wa kuacha mijadala isiyo na tija mitandaoni na kuanza kuangalia "dhahabu" iliyopo mikononi mwetu. Ukiangalia kwa haraka Tanzania imejipambanua kuwa na bidhaa tano ambazo zina uwezo wa kumtoa kijana mmoja mmoja au kwa vikundi kutoka kwenye umasikini na kuwa tajiri wa kimataifa.

 Dhahabu ya Njano: Asali ya Nyuki

China ina kiu kubwa ya bidhaa za asili (organic). Kijana anayeweza kusindika asali ya Tabora au Katavi na kuifunga kwa viwango vya kimataifa, hana mpinzani. Kupitia elimu ya ufundi (VETA) na mitaji ya kizalendo, hili ni zao la kwanza la ushindi.

Mapinduzi ya Viungo (Spices)

Zanzibar na Tanga ni bustani ya dunia. China haitaki tu tangawizi, inataka tangawizi iliyosindikwa au mafuta yake (Essential oils). Huu ni ujuzi unaoweza kumpa kijana heshima na fedha za kigeni.

Parachichi: "Green Gold"

Kwa sasa, parachichi la Tanzania limeanza kutikisa soko la China. Kijana yeyote mwenye ekari moja ya shamba Mbeya au Njombe, anayo tiketi ya kuingia kwenye uchumi wa kimataifa ikiwa atafuata miongozo ya ubora ya TAHA na Serikali.

Bidhaa za Ngozi na VETA

Badala ya kuuza ngozi ghafi, vijana waliopikwa VETA wanaweza kutumia teknolojia ya kisasa kutengeneza viatu, mikanda na mabegi yenye utambulisho wa Kitanzania. Soko la China linathamini sana bidhaa za mikono (handicrafts) zenye asili ya Afrika.

Sanaa na Utamaduni

Vinyago vya Kimakonde na ushanga wa Kimaasai ni bidhaa adimu China. Kupitia masoko ya kidijitali (E-commerce), kijana wa Kitanzania anaweza kuuza sanaa hizi moja kwa moja Beijing bila kupitia dalali yeyote.

Kwa hiyo Tanzania ina kila kitu—kuanzia asali bora, viungo vya Zanzibar, hadi mazao ya bustani. Kinachohitajika sasa ni uthubutu na uwezeshaji wa kitaalamu ili kuhakikisha fursa hii haibaki kuwa "ndoto kwenye karatasi," bali inageuka kuwa utajiri halisi kwa Watanzania.

Jibu kwa Wanaoponda Serikali:

Tuelewane hapa: Serikali kazi yake ni kuchonga barabara na kufungua milango ya kidiplomasia. Hii ya China ni mlango uliokwisha funguliwa. Sasa, kijana anayekaa kijiweni na kusema "Serikali haifanyi kitu" wakati China inasubiri asali yetu bila ushuru, huyo si tu ni zuzu, bali ni mzushi anayekataa fursa kwa makusudi akingojea mana ishuke.

Watanzania wanaoitakia mema nchi yao lazima waone kuwa Serikali imeshatengeneza mazingira—kuanzia hospitali za kibingwa (kama Muhimbili ilivyopokea ujumbe wa Comoro) hadi viwanda na masoko ya nje. Wanaopotosha juhudi hizi mitandaoni ni wazushi wasiojua kuwa dunia inatutazama Tanzania kama kitovu kipya cha uchumi Afrika.

"Dawa ni kujiajiri huku ukiwa umeshaandaliwa kushindana," huu ndio ujumbe mkuu kwa kijana wa leo. Soko la China liko wazi, je wewe uko tayari?


No comments