ITHIBATI KIGEZO KIKUU SAMIA KALAMU AWARDS




Waandishi wa Habari watakaoshiriki Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo (Samia Kalamu Awards - SKA) 2026 wanalazimika kukidhi sharti la kuwa na ithibati kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kukidhi moja ya vigezo vya ushiriki.

Akifafanua wakazi wa uzinduzi rasmi wa mchakato wa kupokea kazi za kushindanishwa, Jumapili Mei 31, 2026, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa SKA, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) , Peter Mwasalyanda, amesema ingizo hilo limewekwa ili kuhakikisha uadilifu, uwazi na ushindani wa haki.

Maandalizi ya tuzo hizo mwaka huu yanahusisha pia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kama mdau muhimu katika kusimamia weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, ili kuhakikisha uwepo wa uadilifu,uwazi na ushindani wa haki. 

Jambo jingine kubwa katika tuzo za mwaka huu ni kwamba alama 40 za ushindani zitatoka kwa majaji wakati wananchi wanachukua alama 60.

Tuzo hizi kwa mara ya kwanza ziliandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).

Aidha amesema  maandalizi ya tuzo za mwaka huu yanazingatia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kutambua mchango wa Waandishi wa Habari za maendeleo nchini.

Tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa Desemba mwaka huu, ni jukwaa mahsusi la kutambua, kuenzi na kukuza weledi katika taaluma ya uandishi wa habari nchini.

Malengo makuu ya tuzo hizo ni kuimarisha ubora wa taarifa, kuongeza uandishi wa maudhui ya ndani yenye tija, kuhamasisha uwajibikaji, kuthamini uzalishaji wa kazi bora zinazochangia kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha, pamoja na kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kulitangaza taifa na kuimarisha taswira chanya ya nchi ndani na nje kupitia habari za maendeleo. 

Kwa mwaka 2026, kamati imejipanga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika msimu uliopita kwa kuhakikisha jukwaa hilo linaendelea kuibua kazi bora zinazochangia maendeleo ya Taifa. 

Dk Kaale


Mwenyekiti wa TAMWA, Dk. Kanaeli Kaale, alihimiza waandishi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwa sababu wao ni daraja muhimu kati ya serikali na wananchi katika kutangaza maendeleo ya nchi, huku Kaimu Mkurugenzi wa JAB,Wakili Patrick Kipangula, akisisitiza washiriki wawe wamethibitishwa na bodi hiyo na wawasilishe habari zenye tija.

“Mtakumbuka Msimu wa kwanza wa Samia Kalamu mambo ya JAB hayakuwepo, kwa hiyo waandishi walishiriki wote bila kujali vigezo vya Ithibati lakini mwaka huu kuna hiki kigezo cha kuwa na ithibati kwa hiyo niwashauri basi wote wanaoshiriki kwenye hizi tuzo wahakikishe wanakuwa na ithibati, wamethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.” Amesema Wakili Kipangula na kuongeza:“Ni muhimu sana kwa sababu ni takwa la kisheria na kitu ambacho hatuwezi kukikwepa. Nawahamasisha tushiriki wote kwa sababu isionekane ni tuzo za watu fulani tu, kila mmoja awasilishe kazi zake.”.



Kwa mujibu wa vigezo vya ushiriki vilivyotangazwa, Waandishi wa Habari wa Tanzania Bara wanatakiwa kuwa wamethibitishwa na JAB, huku kwa Zanzibar washiriki wakitakiwa kuwa na kitambulisho cha Mwandishi wa Habari (Press Card).Mwasalyanda alibainisha kuwa mchakato wa kupokea kazi umeanza rasmi Mei 31, 2026 na utahitihimishwa Juni 30, 2026 kupitia tovuti ya tuzo ambayo ni https://samiaawards.tz ambapo kazi zitakazopokelewa ni zile zilizochapishwa au kurushwa kuanzia tarehe Moja Julai 2025 hadi tarehe 30 Juni 2026. 

Vigezo vya ushiriki vinamtaka mshindani kuwa raia wa Tanzania, asiwe na rekodi ya kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai, na kwa upande wa Tanzania Bara awe amethibitishwa na JAB wakati kwa upande wa Zanzibar awe na kitambulisho cha mwandishi wa habari. 

Kazi inayowasilishwa lazima iwe imechapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza katika vyombo vya habari vya ndani au nje ya Tanzania, iwe imefanyiwa utafiti wa kina unaohusisha uchambuzi na takwimu, na iwe imehusisha vyanzo vya habari visivyopungua vinne bila kuwahi kushindanishwa katika tuzo nyingine yoyote. 

Aidha, habari hizo zinapaswa kuhusu masuala ya maendeleo na kuibua simulizi za wananchi zinazoonesha namna miradi ya kitaifa ilivyofungua fursa na kubadili maisha yao, huku maudhui yake yakizingatia ulinzi wa hakimilili na haki shiriki, na kwa upande wa vyombo vya habari vinavyoshiriki ni lazima viwe na leseni hai iliyotolewa na mamlaka husika.

Tuzo hizi zitahusisha makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalumu za Kitaifa, Tuzo kwa Vyombo vya Habari na Tuzo za Kisekta, zikigusa nyanja mbalimbali za uandishi na utangazaji. 

Katika kundi la vyombo vya habari, kutakuwa na Tuzo ya Chombo cha Habari Mahiri cha Kitaifa itakayotolewa kwa mshindi wa jumla kwa vyombo vyote nchini kwa kutangaza au kuchapisha habari za maendeleo kwa weledi na uendelevu, ikifuatiwa na tuzo maalum kwa Chombo cha Habari Mtandaoni, Magazeti na majarida, Redio za Kijamii zilizopo ngazi ya jamii, Redio za Kitaifa, pamoja na vituo vya Televisheni.





 Upande wa watendaji na waandishi binafsi utahusisha Tuzo ya Mwandishi wa Habari Mahiri kwa aliyefanya vizuri zaidi kwa ujumla katika kategoria mbalimbali, Tuzo ya Afisa Habari Mahiri wa Serikali aliyetangaza au kuchapisha habari na makala za maendeleo na kuwezesha wanahabari kupata taarifa kwa wakati, Tuzo ya Mchoraji Mahiri wa Habari za Katuni, Mwandishi Mahiri wa Habari za Picha, pamoja na Mwandishi Mahiri wa Tahariri.

Kupitia Tuzo za Kisekta, waandishi wa habari mahiri watatambuliwa kulingana na maeneo yao ya msisitizo kijiografia na kisekta, ambapo kwa Tanzania Bara kutakuwa na tuzo maalum za sekta ya Afya, Ardhi na Makazi, pamoja na Elimu, wakati kwa upande wa Zanzibar kukiwa na tuzo za sekta ya Afya, Ardhi, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Elimu na Mafunzo ya Amali, pamoja na Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo. 

Pia kuna tuzo zitakazoshindaniwa kwa sekta nzima nchini zikijumuisha Diplomasia, Fedha na Uchumi, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Kazi na Ajira, Kilimo, Madini, Maji kwa Tanzania Bara, Maji kwa Zanzibar, Maliasili na Utalii kwa Tanzania Bara, Mazingira, Mifugo na Uvuvi, Nishati, Sheria, Siasa, TEHAMA na Ubunifu, Uchukuzi, Uchumi wa Buluu, Ujenzi, Usalama wa Raia, Utalii na Mambo ya Kale kwa Zanzibar, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Utawala Bora, Uwekezaji, Vijana, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa Zanzibar, Viwanda na Biashara, pamoja na kategoria muhimu inayohusu uandishi wa habari mahiri kuhusu haki za Watu wenye Ulemavu.


No comments