AMANI NA UTULIVU NDIO NGUZO KUU YA MAENDELEO YA TANZANIA




Mdau wa maendeleo nchini, Isamilo Zephaniah, ametoa rai kwa Watanzania kutambua kuwa amani na utulivu ndio msingi mkuu wa maendeleo ya taifa, huku akisisitiza kuwa chimbuko la amani hiyo linapaswa kuanzia katika ngazi ya familia. 

Akizungumza juu ya umuhimu wa tunu hiyo, Zephaniah alibainisha kuwa ni wajibu wa kila familia kuanza kufundisha amani, upendo, na utulivu , kwani bila misingi hiyo nyumbani, ni vigumu kupata maendeleo ya kweli au kutekeleza mipango yoyote ya kimaendeleo katika jamii.

Alifafanua kuwa umoja na upendo ndio dira ya safari ya maendeleo ya Tanzania, na kwamba nchi yenye amani hupata nguvu na heshima kubwa mbele ya mataifa mengine. 

Kwa mujibu wa Zephaniah, mazingira tulivu ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje, jambo linalochochea mzunguko wa fedha na kuongeza mapato ya kodi kwa serikali. Alisisitiza kuwa jamii yenye amani hupiga hatua kwa haraka katika nyanja za elimu na biashara, kwani watoto na vijana hupata fursa ya kwenda shuleni na vyuoni bila hofu ya vurugu zinazoweza kusababisha kufungwa kwa taasisi za elimu.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Mkoa wa Pwani, Filemon Maliga, aliyeeleza kuwa amani ndio mtaji mkuu wa wafanyabiashara wadogo. 

Maliga alisema kuwa licha ya mahitaji mengine ya kibiashara, amani inabaki kuwa kipaumbele kwa sababu wawekezaji na wateja wanahitaji utulivu ili waweze kufanya manunuzi na kuendesha shughuli zao kwa usalama. Alitoa wito kwa wananchi kudumisha mshikamano uliopo ili kulinda maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Naye Joyce Mramba, mfanyabiashara katika Soko la Michonjo Uyaoni mkoani Pwani, alibainisha kuwa amani ni uhai wa shughuli zao za kila siku kwani inawawezesha kutoka kwenda kutafuta riziki bila wasiwasi. Aliongeza kuwa kuvunjika kwa amani kunaweza kusababisha washindwe kurejesha mikopo ya biashara walizochukua, jambo linaloweza kurudisha nyuma ustawi wa familia zao. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa soko hilo amewataka vijana kujiepusha na makundi yanayoweza kuhatarisha usalama, akisisitiza kuwa kulinda amani ni jukumu la kila mwananchi bila kujali tofauti zilizopo.

Kutokana na hali hiyo, wadau hao wameihimiza jamii kuendelea kumuunga mkono Rais na viongozi wa serikali ambao wamekuwa wakitimiza wajibu wao kwa vitendo ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha amani. Walihitimisha kwa kusema kuwa umoja unawapa nguvu ya kushinda changamoto za maisha, na hivyo kuna haja ya kuweka maslahi ya Tanzania kwanza kabla ya jambo lingine lolote kwa ajili ya ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.


No comments