TAFFA YAONGEZA MUDA WA KUPIGA KURA, USIKU WA TUZO KUTIKISA DAR
Kutokana na mwitikio mkubwa na shauku ya mashabiki wa filamu kote nchini, Tuzo za Filamu Tanzania maarufu kama TAFFA zimeongeza siku mbili zaidi kwa ajili ya upigaji kura za wasanii na kazi wanazozipenda.
Hatua hii inalenga kutoa fursa pana kwa Watanzania wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika kuwachagua washindi wa tuzo hizo zinazoratibiwa na Studio 19 kwa ushirikiano na Bodi ya Filamu Tanzania.
Mratibu wa tuzo hizo kutoka Studio 19, Brian Paul, amebainisha kuwa mwisho wa kupiga kura sasa utakuwa tarehe 8 Februari ambapo umma unahimizwa kutumia muda huo wa ziada kuhakikisha sauti zao zinasikika kwa kuwapigia kura wasanii wanaowaunga mkono kupitia tovuti rasmi ya tamasha hilo.
Wakati huohuo, Kamati ya TAFFA imetangaza kuwa maandalizi ya Usiku wa Tuzo yamekamilika kwa ajili ya tukio hilo litakalowakutanisha wasanii, watayarishaji, wadau wa sekta binafsi na viongozi wa serikali.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, amesisitiza kuwa tuzo hizo ni kubwa na zinasimamiwa na serikali ili kutoa thamani na mwendelezo wa tasnia ya filamu nchini.
Dkt. Kasiga ameeleza kuwa maandalizi yako vizuri na ushindani ni mkubwa, huku akitambua mchango wa waandishi wa habari katika kuhakikisha vipaji vya wanatasnia vinafika kwa watazamaji kote nchini.
Kilele cha tuzo hizo kinatarajiwa kufanyika tarehe 14 Februari 2026 katika ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam.
Waandaaji wamewahimiza mashabiki kununua tiketi zao mapema kupitia tovuti ya TAFFA ili kushuhudia historia ikieandikwa katika tasnia ya filamu. Kwa mashabiki ambao hawataweza kufika ukumbini, tukio hilo litaonyeshwa mubashara kupitia chaneli ya Sinema Zetu ndani ya Azam TV pamoja na Crown TV ili kutoa nafasi kwa Watanzania wote kushuhudia sherehe hiyo ya vipaji na ubunifu.
Mkurugenzi Mwenza wa Studio 19 amewashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha mchakato huo wakiwemo Benki ya CRDB na Crown FM huku akiwaalika wananchi kujitokeza kwa wingi kusherehekea siku ya wapendanao kwa namna ya kipekee kupitia sanaa ya filamu.

Post a Comment