Tanzania Yaivuta Kampuni Kubwa ya Mafuta Duniani Kuwekeza Nchini
Diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupata mafanikio makubwa baada ya kampuni kinara ya sekta ya mafuta na gesi nchini India kueleza nia yake ya kuwekeza nchini.
Kampuni hiyo ya Indian Oil Corporation Limited, ambayo ni miongoni mwa makampuni makubwa zaidi ya nishati duniani, imevutiwa na mazingira rafiki ya uwekezaji na kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Hatua hii imebainika kando ya Maadhimisho ya Wiki ya Nishati nchini India yanayofanyika katika Jimbo la Goa, ambapo ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, umefanya mazungumzo ya kina na uongozi wa kampuni hiyo. Kuvutiwa kwa wawekezaji hawa wa kimataifa si tu ushindi wa serikali katika kutafuta washirika wa maendeleo, bali ni ushindi wa watanzania wote ambao wanaojiandaa kunufaika na fursa za ajira, ujuzi, na upatikanaji wa nishati ya uhakika.
Mkurugenzi wa Mipango na Biashara wa kampuni hiyo, Suman Kumar, ameuambia ujumbe wa Tanzania kuwa ni soko lenye fursa nyingi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mafuta na gesi kunakosababishwa na ukuaji wa miji na ongezeko la watu. Amebainisha kuwa kampuni yao ina nia ya dhati ya kuwa mshirika wa kibiashara katika usambazaji na uchakataji wa nishati, jambo ambalo litaongeza ushindani wa soko na kusaidia upatikanaji wa huduma bora kwa gharama nafuu kwa kila mtanzania.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Salome Makamba amesisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji wa kimataifa na imekuwa ikifanya maboresho makubwa ili kuwavutia wabia wenye uzoefu. Amewahimiza wawekezaji hao kufungua tawi nchini Tanzania na kushiriki katika mfumo wa ununuzi wa pamoja wa bidhaa za mafuta ili kuimarisha usalama wa nishati na kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambayo ni kipaumbele cha serikali kwa sasa.
Ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hili la kimataifa lililokusanya mataifa zaidi ya mia moja ishirini na tano ni ishara ya wazi kuwa dunia sasa inaielewa Tanzania kama kitovu salama cha uwekezaji barani Afrika. Mafanikio haya yanatajwa kuwa msingi muhimu katika kufanikisha malengo ya muda mrefu ya nchi, ambapo ustawi wa jamii na nguvu ya uchumi wa viwanda unategemea kwa kiasi kikubwa utulivu wa sekta ya nishati na mahusiano imara ya kimataifa.
Kampuni hiyo ya Indian Oil ambayo ina makao makuu yake jijini New Delhi na operesheni katika mataifa mbalimbali, inatarajiwa kuleta mapinduzi ya kiufundi na kibiashara nchini. Hatua hii inaashiria kuwa safari ya kuelekea mwaka 2050 inajengwa kwa vitendo, huku nguvu kazi ya kitanzania ikitarajiwa kupata fursa za mafunzo na ajira kupitia miradi mikubwa inayochochewa na diplomasia makini ya rais na serikali yake.

Post a Comment