WIZARA YA VIJANA: KUTOKA MANENO HADI MATOKEO; MASUALA 645 YATATULIWA KWA MWEZI MMOJA




WAKATI mjadala kuhusu uanzishwaji wa Jukwaa la Vijana ukiendelea mitandaoni, Wizara mpya ya Maendeleo ya Vijana imeonyesha kwa vitendo kuwa suluhu ya changamoto za vijana nchini inategemea kasi ya utendaji na siyo malumbano ya vifungu vya sheria.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Ndugu Joel Nanauka, ameweka wazi kuwa katika kipindi cha mwezi, Desemba pekee, ofisi yake imepokea na kushughulikia masuala 645 yaliyowasilishwa na vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Katika taarifa yake, Waziri Nanauka alisisitiza kuwa Desemba umekuwa ni mwezi wa kazi na siyo maneno. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa changamoto kubwa zinazowakabili vijana ni pamoja na uhitaji wa ardhi kwa uwekezaji, ukosefu wa ajira, changamoto za mikopo ya elimu ya juu, na migogoro ya kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akielezea mifano ya utatuzi huo, Waziri alimtaja mjasiriamali Abdul Juma wa Kibaha ambaye alikuwa akikwama kupata ardhi ya uwekezaji. Kupitia wizara hiyo, kijana huyo aliunganishwa moja kwa moja na Mamlaka ya Uwekezaji (TISEZA). Vilevile, mjasiriamali Baraka Simon wa Dodoma, ambaye biashara yake ilifungwa na TRA kimakosa, alisaidiwa na biashara hiyo ikafunguliwa ndani ya muda mfupi baada ya uhakiki wa taarifa za kodi.

Ufanisi huu unatoa jibu kwa hoja zilizotolewa hivi karibuni na Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, ambao wamekuwa wakipinga Jukwaa la Vijana kwa madai ya kukosa msingi wa kisheria. Hata hivyo, matokeo haya ya wizara yanaonyesha kuwa vijana wanahitaji mfumo unaoweza kufikika (accessible) na unaotumia teknolojia kutatua kero zao sasa hivi.

Kwa upande wa ajira, wahitimu 13 waliokuwa wakikwama kwenye mfumo wa "Ajira Portal" walitatuliwa changamoto zao baada ya kuunganishwa na wataalamu wa TEHAMA wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma. Hatua hizi za haraka zimeonyesha kuwa serikali imejikita kwenye "falsafa ya matokeo."

Kushuka Kwenye Vijiwe na Sokoni 

Waziri Nanauka alibainisha kuwa amefanya ziara katika mikoa ya Mbeya, Songea na Songwe, ambako alikutana na vijana sokoni na kwenye vijiwe vya bodaboda. Katika ziara hizo, aligundua kuwa vijana wengi wanakatishwa tamaa na kukosa nafasi ya kusikilizwa na kucheleweshewa masuala yao katika ofisi za umma.

"Nilikuta kukosekana kwa uwiano wa taarifa za fursa... jambo linalowakatisha tamaa vijana na kujenga chuki miongoni mwao," alisema Nanauka na kuongeza kuwa falsafa yake ni kufanya mambo kwa kasi, kufikika na kutumia teknolojia.

Kuanzishwa kwa wizara hii na hatua hizi za sasa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akihutubia Bunge la 13, ambapo aliahidi wizara maalumu itakayoshughulikia changamoto za vijana, ikiwemo ukosefu wa ajira.

Wakati upinzani ukiendelea kusisitiza sheria namba 12 ya mwaka 2015 ya Baraza la Vijana, takwimu za sasa zinaonyesha kuwa Jukwaa la Vijana na kasi ya wizara ndiyo nyenzo inayotoa majibu ya haraka kwa kijana aliyeko mtaani leo.

No comments