Wito umetolewa kwa vijana wa Tanzania kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani hii.




Vijana wanatakiwa kuelewa kuwa bila amani, maendeleo ya kiuchumi na umiliki wa rasilimali asili haviwezi kufikiwa, hivyo wanapaswa kuwa walinzi wa kwanza wa utulivu wa nchi yao na kanda kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa mafunzo ya Polisi Jamii yaliyofanyika mkoani Mwanza hivi karibuni ambapo, maafisa polisi jamii wamehimizwa kusambaza elimu ya ulinzi shirikishi, kupinga ukatili wa kijinsia, na kubuni miradi bunifu ya kuimarisha usalama. 

Katika mkakati wa kuimarisha utulivu wa ndani wakati kanda ikikabiliwa na mabadiliko ya kisiasa, viongozi wa serikali na wasomi wametoa wito wa kuimarishwa kwa amani, wakibainisha kuwa usalama wa nchi unategemea ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya dola.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dennis Londo, amewaomba viongozi na wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuendeleza utulivu na amani, akibainisha kuwa mkoa huo ni wa kimkakati kwa usalama wa taifa. 

Akizungumza Januari 7, 2026, alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Londo alisisitiza kuwa ufanisi wa vyombo vya ulinzi na usalama unategemea ushirikiano wa wananchi. Mkoa wa Morogoro una umuhimu wa kipekee kwani unatajwa kama ghala la taifa la chakula na chanzo cha huduma mbalimbali kwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima, ameishukuru Serikali kwa maboresho ya sekta ya usalama na kuomba kuendelezwa kwa miundombinu ya magereza. 

Katika kuimarisha ulinzi katika ngazi ya chini, Kamishna wa Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile, amewataka Maafisa wa Polisi Jamii kuimarisha uwajibikaji kwa kutoka maofisini na kwenda kuwahudumia wananchi moja kwa moja katika jamii. Shilogile ameeleza kuwa dhana ya Polisi Jamii hujenga uhusiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, hali inayosaidia kubaini na kuzuia uhalifu mapema.

Kuhusu siasa za kikanda, Mwanasiasa mkongwe nchini, Hamad Rashid Mohamed, amesema kuwa maeneo mengi duniani yamekumbwa na migogoro ya kikanda kutokana na kukosekana kwa mshikamano na amani kati ya mataifa wanachama. Amewahimiza Waafrika kuendelea kushikamana na kudumisha umoja ili kulinda rasilimali zilizopo barani humo.

Mhadhiri wa Chuo cha Mipango Dodoma, Dkt. Immaculate Gillo, amesisitiza kuwa mataifa ya Afrika yanapaswa kuimarisha jumuiya za kikanda ili kutengeneza nguvu ya maamuzi ya pamoja itakayosaidia kulinda maslahi na rasilimali za bara hilo. Alieleza hayo Januari 8, 2026, akibainisha kuwa umoja wa kikanda ni silaha muhimu katika kulinda uhuru wa kiuchumi na kijamii.


No comments