JAB YATOA ONYO KALI KWA WAANDISHI KUANZA UKAGUZI WA ITHIBATI NCHI NZIMA
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imetoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na shughuli za uandishi wa habari nchini bila kuwa na sifa wala ithibati rasmi, huku ikitangaza kuanza kwa operesheni maalum ya ukaguzi nchi nzima.
Hatua hiyo imekuja kufuatia uchunguzi wa Bodi hiyo ulioainiisha kurejea kwa baadhi ya watu wasio na sifa kutekeleza majukumu ya kihabari mara baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu.
Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB Wakili Patrick Kipangula jana Januari 7, 2026, imesisitizwa kuwa uandishi wa habari ni taaluma rasmi inayosimamiwa kisheria, kimaadili na kwa weledi. Bodi imebainisha kuwa yeyote anayefanya kazi za kihabari bila ithibati anakiuka Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023).
Wanaopaswa Kuwa na Ithibati Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kundi linalopaswa kuwa na ithibati ni pana, likijumuisha Wahariri, waandishi wa habari, waandishi huru (freelancers), wapiga picha, wazalishaji wa vipindi, pamoja na watangazaji wa redio na televisheni wanaofanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Ukaguzi Maalum na Hatua za Kisheria Bodi imetangaza kuwa itaendesha ukaguzi maalum katika vyombo vya habari na maeneo tofauti nchini ili kujiridhisha na sifa za watu wanaotekeleza majukumu hayo. Bodi imeonya kuwa haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu binafsi au taasisi zitakazobainika kuajiri au kuruhusu watu wasio na ithibati kufanya kazi.
"Kuendelea kufanya kazi bila ithibati ni kosa kwa mujibu wa Kifungu cha 50 cha Sheria ya Huduma za Habari. Bodi itachukua hatua dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayokiuka masharti haya," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ithibati si Kikwazo cha Uhuru wa Habari JAB imefafanua kuwa utoaji wa ithibati usitafsiriwe kama kikwazo cha uhuru wa habari, bali ni nyenzo ya kulinda heshima na hadhi ya taaluma hiyo. Lengo ni kuongeza uaminifu wa taarifa zinazotolewa kwa umma na kuwapatia waandishi ulinzi wa kisheria wanapotekeleza majukumu yao.
Bodi imetoa wito kwa watu wote wenye nia ya kufanya kazi za kihabari kuhakikisha wanapata ithibati, wanazingatia maadili na kutumia kalamu zao kulitumikia Taifa kwa kutoa taarifa sahihi na kukuza uwajibikaji.

Post a Comment