Waganda kuwafua Wazanzibar utengenezaji wa filamu kwa kutumia simu



Katika jitihada za kuongeza ufanisi na weledi kwenye tasnia ya filamu visiwani Zanzibar, Umoja wa Wazalishaji Filamu Zanzibar (Film Producers Guild) umetangaza mafunzo maalumu ya siku tano ya utengenezaji wa sinema kwa bajeti ndogo.

Rais wa Film Producers Guild na mtayarishaji mahiri wa filamu, Salma Adim, amebainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kiufundi wanafilamu wa Zanzibar ili waweze kushindana katika soko la kimataifa.

Mafunzo haya ya kina yamepangwa kuanza rasmi tarehe 05 hadi 09 Januari 2026 katika hoteli ya kihistoria ya Emerson on Hurumzi. 

Programu hii imeweza kufanikishwa kutokana na udhamini wa Emerson Foundation kwa kushirikiana na Makumbusho ya Princess Salme. 

Salma Adim amefafanua kuwa mafunzo haya yanahusisha wanafilamu 15 waliopo Zanzibar pekee ambao wamefika kupitia utaratibu wa uandikishaji wa Film Producers Guild.

Programu hii itasimamiwa na wawezeshaji nguli wenye uzoefu mkubwa katika nyanja mbalimbali za utengenezaji filamu. Patience Katushabe ambaye ni mtayarishaji na mtaalamu wa utamaduni, ataelekeza masuala ya uandishi wa hadithi, ushirikiano, na taratibu za uzalishaji. 

Ali Musoke ambaye ni mtayarishaji na mwongozaji, atakajikita katika uongozaji, sinematografia, uhariri, na uongozi wa ubunifu. Aidha, mtaalamu wa urembo na mavazi Esther Nakaziba, ataongoza vipindi vya uumbaji wa wahusika na usanifu wa mavazi.

Salma Adim ameeleza kuwa hii ni fursa ya kipekee kwa vijana na wataalamu wa Zanzibar kujifunza kuanzia hatua za awali za wazo la filamu hadi hatua ya mwisho ya uandaji. 

Alisisitiza kuwa wamejipanga kuhakikisha kila mshiriki anatoka hapo akiwa na ujuzi mpya utakaobadilisha ubora wa kazi zake. Mafunzo haya yanayoratibiwa chini ya mradi wa Matatu Film Lab na kuwezeshwa na Film Possible, yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika utamaduni wa uandaji filamu visiwani humo.

No comments