SERA SAHIHI, TAIFA IMARA: NSSF YAWAVISHA ‘KINGA’ YA KIUCHUMI VIJANA




KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni matunda ya amani, utulivu, na mipango thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unatekeleza mkakati maalum unaolenga kutoa ulinzi wa kiuchumi kwa vijana wa Kitanzania wanaopata fursa za ajira ughaibuni. 

Mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa nguvu kazi inayokwenda nje haipotezi uhusiano wa kiuchumi na nyumbani, bali inajenga uwekezaji wa kudumu kwa ajili ya mustakabali wa familia zao.

Mkakati huu  ni utekelezaji wa kivitendo wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kulifungua Bunge la 13. 

Katika hotuba yake, Rais Samia aliahidi kuanzishwa kwa Wizara maalum na mifumo madhubuti ya kushughulikia masuala ya vijana, ikiwemo changamoto ya ajira na hifadhi yao, akisisitiza kuwa serikali itahakikisha kila kijana anapata fursa na kulindwa kisheria na kiuchumi.

Utekelezaji wa mkakati huu wa NSSF haujaja kwa bahati mbaya ni kutokana na kuwapo wa mazingira ya amani ya sasa ambapo diplomasia ya kiuchumi imefungua milango ya mataifa mengine kuamini nguvu kazi ya Tanzania. 

Sera sahihi za serikali kuhusu ustawi wa wananchi zimewezesha uanzishwaji wa "Hifadhi Scheme" (National Social Security Scheme for Self Employed), ambayo sasa inakuwa "mwavuli wa usalama" kwa vijana wanaokwenda ughaibuni.

Katika hafla maalum ya kuwaaga vijana 109 waliopata ajira ughaibuni kupitia mawakala 15 wanaofanya kazi kwa karibu na Serikali,NSSF ilitoa elimu na kusajili vijana hao moja kwa moja ili waondoke nchini wakiwa na uhakika wa maisha yao ya baadaye.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Uhusiano wa NSSF, Lulu Mengele, alisisitiza kuwa hifadhi ya jamii ni silaha kubwa kwa kijana anayekwenda kufanya kazi mbali na nyumbani.

"Tunawataka vijana hawa wasiondoke hivi hivi. Kujiunga na NSSF kupitia Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi kutawawezesha kujiwekea akiba ambayo itawalinda dhidi ya majanga, kutoa bima ya matibabu kwa familia wanazoziacha, na muhimu zaidi, kuwa na uhakika wa maisha pindi mikataba yao itakapokamilika na kurejea nchini," alisema Mengele.

Alifafanua kuwa kipato kinachopatikana nje kinapaswa kuwa chachu ya uwekezaji nchini. Kupitia NSSF, mwanachama anajihakikishia mafao ya uzazi, matibabu, ulemavu, na msaada wa mazishi, huku akipata fursa ya kuchukua sehemu ya michango yake (mafao ya kujitoa) kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo hapa nyumbani.

Mkakati huu umekuwa rafiki zaidi kutokana na matumizi ya teknolojia, jambo ambalo serikali imeliwekea mkazo. Ili kujiunga, kijana anahitaji tu Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA). Huduma zote kuanzia usajili, ulipaji michango kuanzia Sh 30,000 au 52,200 kwa mwezi, hadi uhakiki wa salio, zinafanyika kiganjani kupitia mfumo wa (ARAFA-USSD) *152*00# au NSSF Portal. Hii inamwezesha kijana aliyeko ughaibuni kusimamia akaunti yake akiwa popote duniani bila urasimu.

Mkakati huu wa NSSF ni hatua kubwa katika kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kupunguza umaskini na kukuza nguvu ya uzalishaji. Amani na utulivu uliopo nchini unazidi kuwa "dau" muhimu katika kufungua milango ya kimataifa.

Kama alivyoelekeza Rais Dkt. Samia bungeni, serikali imejipanga kuhudumia wananchi wake popote walipo. NSSF sasa imesimama kama mlinzi wa kiuchumi wa vijana hawa, ikithibitisha kuwa ughaibuni siyo mahali pa kupoteza mafao, bali ni uwanja wa kuzalisha mali huku serikali ikilinda ustawi wako na wa familia yako nyumbani.

No comments