Samuel Eto’o achapwa faini ya Sh milioni 56 na CAF kwa utovu wa nidhamu
Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limemshushia rungu zito Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto’o, kwa kumfungia kutojihusisha na soka kwa mechi nne pamoja na faini ya Dola 20,000 (takriban Shilingi milioni 56 za Kitanzania).
Adhabu hiyo inakuja kufuatia vitendo vyake vya utovu wa nidhamu baada ya Cameroon kukubali kichapo kutoka kwa Morocco katika hatua ya robo fainali ya AFCON 2025.
Nini kilitokea jukwaani?
Eto’o, ambaye alikuwa akitazama mechi hiyo jukwaani, alionekana akizozana kwa hasira na Rais wa Shirikisho la Soka la Morocco, Fouzi Lekjaa, pamoja na Rais wa CAF, Patrice Motsepe. Tabia hiyo ilitafsiriwa kama utovu wa nidhamu uliopitiliza na chombo hicho kinachosimamia soka barani Afrika.
Hata hivyo, mambo hayakuishia hapo. Nchini Cameroon, mjadala mkali umekuwa ukiendelea kuhusu maamuzi ya mwamuzi, hususan tukio lililomuhusisha mshambuliaji Bryan Mbeumo, ambalo mashabiki wa Cameroon wanaamini walionewa.
Cameroon wagoma, wasema "Hatukubali!"
Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT) limepinga vikali adhabu hiyo likidai kuwa ni kubwa mno na haitendeki haki. Katika taarifa yao rasmi, FECAFOOT imesema:
"Hatuelewi msingi wa uamuzi huu wa CAF. Utaratibu uliotumika kutoa adhabu hii ni wa kukurupuka na haukuzingatia misingi mikuu ya haki kwa mtuhumiwa kujitetea."
Uchunguzi mwingine waanzishwa
Wakati sakata la Eto'o likipamba moto, CAF imetangaza pia kuanzisha uchunguzi mwingine kuhusu mechi kati ya Algeria na Nigeria. Hii ni kufuatia vurugu na matukio yasiyo ya kimichezo yaliyotokea mara baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo.

Post a Comment