Mradi wa Bomba la Mafuta la EACOP na Uwekezaji wa Bandari Nchini: Ajira na Fursa za Kiuchumi Zazidi Kupamba Moto
Utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ujenzi wa bandari na miundombinu ya nishati kote nchini umeendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na mapato kwa Watanzania, ambapo mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) pekee ambao umefikia asilimia 79 ya utekelezaji, hadi kufikia Juni 2025, mradi huo ulikuwa umezalisha jumla ya ajira 9,194.
Akizungumza na waandishi wa habari katika bandari ya Dar es salaam Januari 20, Msemaji mkuu wa serikali na Katibu Mkuu wizara ya Habari, sanaa Utamaduni na michezo, Ndugu Gerson Msigwa amesema asilimia 80 ya ajira hizo zimeenda kwa Watanzania, huku kiasi cha Shilingi Trilioni 1.325 kikitumika kununua bidhaa na huduma kutoka kwa makampuni ya ndani zaidi ya 200.
Alisema pamoja na ujenzi wa bomba hilo pia kuna maendeleo mazuri ya ujenzi wa miundombinu mkoani Tanga yanajumuisha kituo cha kupokelea mafuta cha Chongoleani na ujenzi wa matenki manne yenye uwezo wa kutunza mapipa milioni 2, kazi ambayo imefikia hatua za juu za ukamilishaji ikihusisha pia ujenzi wa gati lenye urefu wa kilomita mbili kwa ajili ya kupakilia mafuta kwenye meli.
Sambamba na mradi huo wa bomba la mafuta, Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inaendelea na ujenzi wa bandari mpya kote nchini ikiwemo Bandari ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara inayojengwa mahususi kwa ajili ya shehena za makaa ya mawe na saruji ambayo imefikia asilimia 18.
Katika Kanda ya Ziwa, ujenzi wa Bandari ya Mwanza North umefikia asilimia 80, huku Bandari ya Kigoma ikifanyiwa maboresho makubwa kupitia msaada wa serikali ya Japan na tayari ujenzi wa gati za Kibirizi na Ujiji umefikia asilimia 99. Kukamilika kwa miradi hii ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay ambayo imefikia asilimia 46 kutaimarisha mfumo wa usafirishaji wa mizigo kupitia njia ya reli na maji, jambo litakalopunguza gharama za maisha kwa wananchi na kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi wa ndani.
Post a Comment