Bandari ya Dar es Salaam yawezesha Tanzania kuwa Kitovu cha Biashara Afrika
Nafasi ya Tanzania kama kitovu cha kimkakati cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika imezidi kuimarika kufuatia maboresho makubwa yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo sasa imekuwa lango tegemeo kwa nchi nane jirani.
Takwimu zilizotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali leo zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 pekee, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa nchi inayoongoza kwa kutumia bandari yetu ikisafirisha shehena ya tani 5,995,293, ikifuatiwa na Zambia iliyohudumiwa tani 3,510,706. Nchi nyingine zinazofaidika na ufanisi huu ni pamoja na Rwanda iliyosafirisha tani 1,724,370, Malawi tani 675,200, na nchi nyingine kama Burundi, Uganda, Zimbabwe na mataifa mengine madogo yanayozunguka ukanda wetu.
Ongezeko hili la mzigo ni matokeo ya moja kwa moja ya uwekezaji uliofanywa na serikali na kupangishwa kwa kampuni za DP World na TEAGTL ambao umewezesha kupunguza muda wa meli kusubiri nangani na kuhudumiwa kutoka wastani wa siku 30 hadi kufikia wastani wa siku 6 pekee kwa meli za makasha.
Maboresho ya Gati namba 1 hadi 7 na miradi inayoendelea ya gati namba 8 hadi 11 inaikaribisha Tanzania katika daraja la juu la kiushindani dhidi ya bandari za Mombasa, Maputo na Durban.
Kwa sasa, Bandari ya Dar es Salaam inaandaliwa kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa za kizazi kipya zinazojulikana kama Post Panamax zenye urefu wa hadi mita 305 na uwezo wa kubeba makasha 8,000 kwa wakati mmoja, hatua itakayoiwezesha nchi kufikia lengo la kuhudumia zaidi ya tani milioni 30 za shehena kwa mwaka na kuchochea ukuaji wa kasi wa uchumi wa taifa.
Kwa ujumla alisema uwekezaji uliofanywa na DP World pamoja na TEAGTL mpaka sasa umeleta mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la shehena hadi kufikia tani milioni 27.7 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na tani milioni 23.69 za shehena zilizohudumiwa mwaka 2023/2024.
“Katika kipindi cha miezi sita kinachoanza mwezi Julai hadi Desemba 2025, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia jumla ya tani milioni 16.7 ambazo ni kubwa kwa asilimia 30 ukilinganisha na tani milioni 12.8 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024,” aliongeza Msigwa.
Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, uwekezaji uliofanyika umetoa ajira ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2025, jumla ya wafanyakazi 764 walipata ajira za moja kwa moja katika Kampuni za DP World na TEAGTL katika fani mbalimbali wakiwemo maofisa wa idara mbalimbali, makarani wa shughuli za uendeshaji, waendesha mitambo mikubwa na midogo na askari.
Alisema sambamba na ajira hizo za moja kwa moja, Kampuni ya DP World na TEAGTL zimetengeneza pia ajira nyingine zisizo za moja kwa moja kufuatia ongezeko la shehena mchanganyiko na shehena ya makasha zikijumuisha wafanyakazi wa kutwa, madereva wa malori na mawakala wa forodha.
Post a Comment