Mapinduzi ya Usafirishaji: Reli ya SGR, MGR na TAZARA Kuunganishwa na Bandari ya Dar es Salaam
Serikali imetangaza mpango kabambe wa kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na mifumo ya reli nchini ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kwenda mikoani na nchi jirani kwa kasi.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ameeleza kuwa kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), serikali imeshaingia mkataba na mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya reli ndani ya bandari itakayounganisha reli ya mita (MGR), reli ya kisasa (SGR), na reli ya TAZARA. Lengo la mradi huu ni kuondoa msongamano wa malori barabarani na kuhakikisha mizigo inafika kwa haraka na usalama zaidi.
Uchambuzi wa tija ya mradi huu unaonesha kuwa ukikamilika, utaongeza uwezo wa kuhudumia shehena ya makasha hadi kufikia makasha 480,000 kwa mwaka.
Hali kadhalika, mradi huu utaleta mageuzi ya kihistoria katika sekta ya uchukuzi nchini ambapo usafirishaji wa shehena kwa njia ya reli unatarajiwa kuongezeka mara sita, kutoka asilimia 2 ya sasa hadi kufikia asilimia 12.
Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango kuu la kiushindani katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ikizichuana na bandari za Mombasa na Durban kwa kutoa huduma za kisasa za usafirishaji wa njia mchanganyiko.
Post a Comment