WANASEMAJE MTANANGE WA TAIFA STARS NA SUPER EAGLES
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kinaingia uwanjani kesho Jumanne huko Fes, Morocco, kikiwa na dhamira ya kuandika historia mpya katika mashindano ya mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Chini ya kocha Miguel Gamondi, Tanzania inasaka ushindi wake wa kwanza kabisa katika fainali hizi baada ya kushiriki mara tatu huko nyuma bila mafanikio ya pointi tatu.
Katika kile kinachoonekana kama mwanzo wa zama mpya, Stars imeweka kambi ya nguvu nchini Misri kabla ya kutua Morocco, ikijipanga kuvunja mwiko dhidi ya miamba ya soka barani Afrika, Nigeria.
Gamondi anatarajiwa kujenga mtego wake wa ushindi kupitia uzoefu wa nahodha Mbwana Samatta anayekipiga Ufaransa na Simon Msuva, huku akitegemea ubunifu wa kiungo Feisal Salum na ulinzi imara wa pembeni kutoka kwa Mohamed Hussein. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufuzu fainali hizi mara mbili mfululizo, jambo linalotoa ishara kuwa timu hiyo imekomaa na iko tayari kupambana na yeyote.
Kwa upande mwingine, Nigeria maarufu kama Super Eagles, wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na njaa ya mafanikio baada ya kupoteza fainali iliyopita dhidi ya Ivory Coast.
Wakiwa wamefanya mazoezi makali mara nne tangu walipowasili Morocco, mabingwa hao mara tatu wa Afrika wanapigiwa upatu mkubwa kutokana na ukubwa wa kikosi chao chenye mastaa kama Victor Osimhen na Ademola Lookman.
Historia inaibeba Nigeria kwani haijawahi kupoteza mchezo dhidi ya Tanzania mara saba iliyopita, huku kumbukumbu ya mwisho ya timu hizi kukutana katika AFCON ikiwa ni mwaka 1980 ambapo Nigeria ilishinda mabao matatu kwa moja. Hata hivyo, hali ya kikosini kwa Tanzania inaonekana kuwa na utulivu mkubwa, na wachezaji wameahidi kupambana kufuta uteja huo wa miaka 45 dhidi ya Wanigeria.
Mchezo huu wa Kundi C utakaopigwa katika uwanja wa Complex Sportif de Fes, unatarajiwa kuwa wa mbinu nyingi. Wakati Nigeria wakisaka kufikisha mabao 150 katika historia yao ya AFCON, Taifa Stars inalenga kulinda lango lake na kutumia mashambulizi ya kushtukiza ili kuwashangaza wapinzani wao.
Uwepo wa kipa wa Nigeria, Amas Obasogie, anayecheza soka nchini Tanzania katika klabu ya Singida Black Stars, unaongeza ladha ya kipekee kwenye mtanange huu kwani anawafahamu vyema wachezaji wengi wa Tanzania.
Watanzania wanasubiri kwa hamu kuona kama Gamondi ataweza kuishangaza Afrika kwa kuwatoa nishai Super Eagles katika mchezo huu wa ufunguzi.


Post a Comment