Utii kwa mamlaka ni takwa la Mungu, Kibwana aonya kauli za wanasiasa
Kumekuwepo na wito kwa Watanzania kutumia umoja na amani kama msingi wa kupigania uhuru kamili wa kiuchumi na kuacha tabia ya kutegemea misaada ya nje kutatua matatizo ya ndani. Wito huu unaambatana na msisitizo wa kuitii Mamlaka ya Rais kama njia ya kuhakikisha utulivu wa taifa.
Geofrey Kiliba, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO), amewaomba Watanzania kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake, pamoja na kuwaombea ili waweze kutumikia wananchi kikamilifu.
Akizungumza Dar es Salaam, Kiliba alikumbusha umuhimu wa kuwatii viongozi kama inavyoelekezwa na maandiko matakatifu.
"Hili ni takwa la Mwenyenzi Mungu kupitia maandiko matakatifu, sisi Wakristo imeandikwa kwenye Warumi 13:1: 'Kila mtu na atii mamlaka kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mwenyenzi Mungu.' Kutokutii ni kupishana na maagizo ya Mwenyenzi Mungu," alisema Kiliba.
Kiliba alisisitiza kuwa utii kwa mamlaka ya Rais ni muhimu kwa manufaa ya nchi, akimaanisha heshima kwa urais inasaidia kuimarisha utawala na kuepuka aibu ya kutafuta suluhisho la matatizo yetu kutoka nje ya mipaka yetu.
Wanasiasa wahimizwa Kuimarisha Umoja
Wakati huo huo, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Thomas Kibwana, ametoa rai kwa wanasiasa nchini kuhakikisha kauli wanazozitoa zinakuwa chachu ya kuimarisha umoja wa kitaifa, kuunganisha jamii na kuhamasisha amani, uzalendo na uwajibikaji. Alisema kauli zinazochochea chuki na migogoro hazipaswi kupewa nafasi.
Akizungumza kupitia TBC1, Kibwana alibainisha kuwa siasa nchini zinapaswa kujikita zaidi katika kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi, kwani hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda na kuimarisha amani ya nchi.
Wito huo unaungwa mkono na hisia za vijana wengi ambao wamethibitisha kujitolea kwao kwa amani.
"Amani imeshinda. Katika nchi yetu, sauti ya utulivu imezidi kelele za chuki, propaganda na miito ya uasi," alisema mmoja wa vijana. "Vijana wa Tanzania tumethibitisha kuwa nguvu yetu kubwa si vurugu, bali busara, umoja na upendo kwa taifa letu."
Kwa mujibu wa Mwalimu Julius Nyerere, "Umoja wetu ndio nguzo ya msingi ya mafanikio yetu." Kwa kuheshimu viongozi na kudumisha utulivu, Watanzania wanaweka msingi imara wa kujitawala kiuchumi na kuondoa aibu ya kutegemea nje.

Post a Comment