Hasara za Vurugu za Oktoba 29 Zinatishia Safari ya Uhuru wa Kiuchumi




Matukio  ya vurugu za Oktoba 29, yameibua wasiwasi kwa Taifa kutokuwa na kasi ya kufikia malengo yake ya uhuru kamili wa kiuchumi ifikapo 2050. DIRA 2050 inajengwa kwenye misingi ya amani, utulivu, na ushirikiano wa wananchi, na matukio hayo yameanza kuonyesha gharama halisi za uvurugaji wa amani.

Kufuatia vurugu za Oktoba 29, sauti za wananchi zimeanza kusikika zikieleza  uhalisia kwamba uvurugaji wa amani unakwenda kinyume na malengo makuu ya DIRA 2050 kwa kupunguza kasi iliyokusudiwa na kuumiza maisha ya kila siku ya wnanchi ambao uwakilishi wao wa kiuchumi ni pamoja na kutyoka kila siku kupata mahitaji yao.

Bw. Juma Mussa, Mfanyabiashara Ndogo, Kariakoo anasema:"Mimi sitaki DIRA 2050 iwe maneno matupu. Nataka ionekane kwenye mfuko wangu. Siku zile za vurugu, soko lilifungwa. Nilisimama bila kuuza, nikatoka na hasara. Hii inatupunguza mwendo wa kiuchumi, sisi ndio injini! Serikali inapoteza kodi, sisi tunapoteza mtaji."

Mama Amina Selemani, Mjasiriamali, Arusha anasema: "Ni huzuni sana kuona vijana wetu wanaharibu miundombinu. Barabara zikiharibika au ofisi zikichomwa, nani anabeba gharama? Ni kodi zetu zinazotakiwa kujenga shule na zahanati, zitaenda kurekebisha uharibifu. Tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Amani ndio ufunguo wa huu uchumi wa dola trilioni 1 ambao Rais Samia anauzungumzia."

Dkt. Neema Charles, Mchumi na Mwekezaji Mdogo, Dar es Salaam anaongeza kusema:"Kama mwekezaji mdogo, vurugu huleta hofu. Ukiwekeza fedha zako halafu kuna tishio la mali yako kuharibiwa au wafanyakazi wako kukosa usalama, inakufanya uhofie. DIRA 2050 inataka wawekezaji waje; hofu inawafukuza wawekezaji, wa ndani na nje. Hii inatishia lengo letu la kuwa nchi ya kipato cha kati ya juu."

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliweka wazi wakati wa uzinduzi Julai 17, 2025, kwamba: "Yaliyomo katika DIRA 2050 yanaakisi maoni na matakwa ya Watanzania wenyewe. Tumetafakari pamoja, tumepanga pamoja, na tutatekeleza pamoja.”

Falsafa hii ya utekelezaji wa pamoja inakufa wakati vurugu zinapozuka. Waziri Prof. Kitila Mkumbo alisisitiza umuhimu wa DIRA hii kulindwa Bungeni. Lakini ulinzi wa kweli unatokana na utulivu wa kijamii, ambao unahakikisha utekelezaji wa mipango ya kitaifa unaendelea bila kukatizwa.

Vijana wa Tanzania, ambao ni asilimia 65 ya wananchi, ndio chachu ya DIRA 2050. Kila tukio la vurugu huongeza umbali wa kufikia lengo la uhuru wa kiuchumi na linaweza kupunguza kasi ya kufikia uchumi wa dola trilioni 1, hivyo kuhatarisha ustawi wa jamii wa vizazi vijavyo. Amri ya amani inawapa nafasi ya kudumisha maendeleo endelevu.

No comments