Polisi Morocco Wanasa Walanguzi wa Tiketi, Wahujumu Furaha ya Mashabiki



Jeshi la Polisi nchini Morocco limewatia mbaroni watu wanane kwa tuhuma za kuhujumu uuzaji wa tiketi za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), hali iliyosababisha mashabiki wengi kukosa nafasi ya kushuhudia mechi za ufunguzi licha ya viwanja kuwa na nafasi.

Hatua hiyo ya usalama imekuja kufuatia malalamiko makubwa kutoka kwa mashabiki waliokwama kupata tiketi kupitia mifumo rasmi, huku kukiwa na mfululizo wa matangazo ya tiketi hizo kwenye mitandao ya kijamii zikiuzwa kwa bei ya juu kinyume na taratibu. Operesheni hiyo kabambe iliyofanyika katika miji ya Rabat, Temara, Agadir, Sale, Marrakech, na Mohammedia, imefanikiwa kuwanasa washukiwa hao ambao walitumia mbinu za kitaalamu kununua tiketi kwa wingi mtandaoni na kisha kuzigeuza kuwa bidhaa ya walanguzi.

Hujuma hiyo imekuwa na athari kubwa kiwanjani, ambapo imebainika kuwa zaidi ya viti elfu kumi vilibaki wazi katika Uwanja wa Moulay Abdellah wakati wa mchezo kati ya wenyeji Morocco dhidi ya Comoro. Hali hiyo imezua simanzi kwa mashabiki waliokuwa tayari kuishangilia timu yao lakini wakashindwa kumudu bei kubwa iliyopangwa na walanguzi hao, ambao wanadaiwa kupandisha bei maradufu ya ile iliyokusudiwa na mamlaka za soka.

Polisi nchini Morocco wamesema kuwa mbinu zilizotumiwa na walanguzi hao zinafanana na zile zilizojitokeza wakati wa Kombe la Dunia kule nchini Qatar mwaka juzi, jambo lililopelekea vitengo vya ufuatiliaji wa makosa ya mtandaoni kuingilia kati. Uchunguzi wa kitaalamu ulibaini kuwa baadhi ya wahusika walikuwa wakitumia akaunti mbalimbali za mitandao ya kijamii kuwanasa mashabiki wenye shauku na kisha kuwauzia tiketi kwa njia zisizoidhinishwa.

Wakati washukiwa hao wakiendelea kuhojiwa ili kuwabaini washirika wao wengine, mamlaka za usalama zimezidi kuwahimiza mashabiki kuwa na subira na kutokubali kununua tiketi nje ya mifumo rasmi. Serikali imeahidi kuwa haitachukua muda mrefu kabla ya mfumo wa uuzaji tiketi kurejea katika hali ya kawaida na kwa bei halali, ili kuhakikisha viwanja vinajaa na mashabiki wanapata haki yao ya kushiriki katika tamasha hilo la soka la Afrika.

No comments