AFCON 2025: Gamondi Agoma Kuwa "Timu Ndogo", Makonda Aipongeza Stars kwa Kuishitua Nigeria
Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Miguel Gamondi, ametangaza vita dhidi ya dhana ya Tanzania kuonekana kama "timu ndogo" barani Afrika, akisisitiza kuwa kikosi chake kimeimarika na kiko tayari kupindua meza ya matokeo katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) zinazoendelea nchini Morocco.
Akizungumza mara baada ya mchezo wa kwanza wa Kundi C ambapo Stars ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya miamba ya soka, Nigeria, Gamondi alisema kuwa licha ya matokeo hayo, uwanjani kuliibuka taswira mpya ya soka la Tanzania. Alibainisha kuwa Stars ya sasa ina uwezo wa kushambulia na kufunga hata inapokabiliana na mataifa makubwa, jambo ambalo limekuwa likikosekana kwa miaka mingi.
"Tumeimarika sana. Leo tumeonyesha kuwa tuna uwezo wa kushambulia na kulazimisha matokeo. Unapocheza na timu kama Nigeria, huwezi tu kushambulia bila mbinu; ni mchezo uliotawaliwa na akili nyingi. Ninataka tuondoe kabisa dhana kuwa Tanzania ni timu ndogo, na kwa maboresho tunayoyafanya, ulimwengu utatuelewa," alisema Gamondi kwa kujiamini.
Kauli hiyo ya Gamondi iliungwa mkono na Kocha Mkuu wa Nigeria, Eric Chelle, ambaye licha ya kuondoka na alama tatu, alikiri kuwa vijana wa Kitanzania walimpa wakati mgumu. Chelle alisema ushindi wao unahitaji tathmini ya kina kwani Tanzania iliweza kutumia makosa yao na kuwatikisa, hususan katika kipindi cha pili cha mchezo huo uliopigwa juzi.
Hali hiyo ya Stars "kutoa jasho" kwa miamba ya soka barani imemvutia pia Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ambaye ameambatana na timu hiyo nchini Morocco. Makonda amewapongeza wachezaji kwa kupigana kishujaa na kulinda heshima ya nchi, akifichua kuwa hata viongozi wa juu wa soka nchini Nigeria wameshangazwa na kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na Stars.
"Kwa vita mliyopigana uwanjani mmeilinda heshima ya Tanzania. Rais wa Shirikisho la Mpira la Nigeria na Waziri wao wa Michezo wamekiri wazi kuwa kile walichokiona uwanjani hawakukitarajia kutoka kwenu," alisema Makonda wakati akizungumza na wachezaji kambini.
Akiangalia mbele kuelekea mchezo muhimu dhidi ya Uganda 'The Cranes' unaotarajiwa kupigwa keshokutwa, Makonda amewataka wachezaji kuongeza bidii akisisitiza kuwa Taifa Stars ina kila sababu ya kutinga hatua inayofuata. Aliongeza kuwa kiwango walichonacho hivi sasa kinawapa jeuri ya kushinda michezo iliyosalia dhidi ya Uganda na Tunisia.
Tanzania, ambayo inashiriki fainali hizi kwa mara ya nne baada ya rekodi za mwaka 1980, 2019 na 2023, inatafuta kuvunja mwiko wa kuishia hatua ya makundi. Katika fainali hizi zitakazotamatika Januari 18, mwakani, macho yote ya mashabiki nchini yapo kwa Gamondi na vijana wake kuona kama watafanikiwa kufuta unyonge wa "timu ndogo" na kuandika historia mpya barani Afrika.

Post a Comment