KISWAHILI CHAPITISHWA KUWA LUGHA RASMI YA UNESCO




Nyota ya Kiswahili imeendelea kuangaza Kimataifa baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuridhia Lugha hiyo kuwa moja ya Lugha  zitakazotumika  Rasmi katika Mikutano Mikuu ya Shirika hilo.

Kauli hiyo imetolewa katika  Mkutano Mkuu wa 43 wa Shirika hilo uliofanyika Samarkand - Uzbekistan kuanzia tarehe 30 Oktoba na unaotarajiwa kuhitimishwa  Novemba 13 mwaka 2025.

Tamko la hilo la  UNESCO  ambalo limetolewa Novemba 11, 2025, limetokana na  maombi yaliyowasilishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Kupitia wizara ya  Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Kwa kushirikiana na Mabaraza ya Kiswahili Tanzania BAKITA na BAKIZA.

Kufuatia hatua hiyo tayari Tanzania imepewa fursa ya kuwasilisha hotuba ya nchi baada ya maombi yake kuridhiwa. hotuba ambayo imetolewa na Mhe. Ali Jabiri Mwadini, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na mwakilishi wa kudumu wa UNESCO.

Kupitishwa kwa Kiswahili kuwa Lugha ya kazi kunafanya Lugha hiyo kuwa ya  kwanza yenye asili ya Afrika kupewa hadhi hiyo huku hatua hii  muhimu ikitarajiwa  kufungua milango mingi  zaidi ya Kiswahili katika taasisi, mashirika ya Umoja wa Kikanda na Kimataifa. 

Aidha, ikumbukwe kuwa, UNESCO Katika Mkutano wake wa 41 wa Novemba 2021 ndio uliopitisha azimio la kuwa na Siku ya Kiswahili Duniani ambayo huadhimishwa  tarehe 7/7 ya Kila Mwaka  na Siku hiyo ilitambuliwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Julai, 2024. 

Hivyo basi unaweza kusema , Kiswahili kwa sasa ni Lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC), Jumuiya ya Wazalishaji Almasi Afrika (ADPA) na Umoja wa Afrika (AU). 

Nafasi hizi za Kiswahili Kimataifa zinatarajiwa kwa kiasi kikubwa  kuimarisha ajira na fursa kwa wataalamu wa Kiswahili katika Ufundishaji, Tafsiri, Ukalimani, Uandishi wa Vitabu na Utangazaji.


No comments