Dkt. Samia Ashukuru Waangalizi wa Kimataifa, Lakini Asisitiza Mamlaka ya Taifa
Chamwino, Dodoma
Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shukrani za dhati kwa waangalizi wote wa uchaguzi kutoka Jumuiya za Kimataifa na Kikanda waliohudhuria siku yake ya kuapishwa.
Alibainisha kuwa ni kawaida kwa nchi zenye mfumo wa Kidemokrasia kualika waangalizi wa uchaguzi. Uwepo wao, alieleza, huongeza uhalali wa juhudi za Taifa la Tanzania katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya uwazi, haki, heshima, na utawala wa sheria.
Rais Samia alizishukuru Jumuiya zote zilizotuma waangalizi wa uchaguzi. Kutoka Afrika, waangalizi walitoka katika Jumuiya zifuatazo:Umoja wa Afrika (AU) ,Jumuiya ya nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) ,Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) .
Pia, kulikuwa na waangalizi wengine kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Rais alithibitisha kwamba makundi yote ya waangalizi tayari yametoa taarifa za awali, na kwamba Serikali imepokea maoni yao kwa heshima kubwa. Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kunukuu kipande cha hotuba ya Hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, wakati akiapishwa kuwa Rais mwaka 2000.Akizungumzia kauli hiyo, Rais Samia alisisitiza msimamo wa Taifa kwa kunukuu maneno haya:
"Nawashukuru watazamaji wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifia tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu. Tumesikia pia waliyodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi tumeyaona. Maagizo yao tumeyakataa, ushauri wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo."
Kauli hiyo inaashiria heshima kwa ushiriki wa kimataifa, huku ikitilia mkazo mamlaka na uhuru wa Taifa la Tanzania kufanya maamuzi yake yenyewe, ikipokea ushauri lakini ikikataa kuamriwa.

Post a Comment