Rais Samia Aahidi Kuwatumikia Watanzania Wote Bila Ubaguzi, Aonya Wachochezi wa Vurugu




CHAMWINO, DODOMA


Baada ya kuapishwa rasmi kwa kipindi cha pili kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa wito wa dhati wa kuwatumikia Wananchi wote bila kujali tofauti zao za kisiasa. 

Alisema kwamba uchaguzi ni fursa kwa Wananchi kueleza matakwa yao ya aina ya viongozi wanaodhani wataweza kuwatumikia vyema na kuwaletea maendeleo endelevu. 

Alisema ingawa kipindi cha kampeni Taifa liligawika kiitikadi na kishabiki, Rais Samia alisisitiza kuwa anayechaguliwa na wengi huwa ndiyo chaguo la nchi na anapaswa kuwa Mtumishi wa Wananchi wote. Hii inajumuisha wale waliomchagua, waliochagua wagombea wengine, na hata wale ambao hawakushiriki uchaguzi.

 Rais aliwahakikishia Watanzania kuwa ahadi yake na ya timu yake ni kulitumikia Taifa hili kwa nguvu zao zote, vipawa vyao vyote, na maarifa yao yote.

Akisisitiza umuhimu wa kuendelea mbele baada ya msimu wa siasa, Rais alikumbusha kuwa uchaguzi mkuu wa Viongozi wa Serikali ni mchakato wa msimu mmoja tu ndani ya miaka mitano. Alieleza kuwa muda mwingine wote, maisha lazima yaendelee, hivyo Jukumu la Watanzania wote ni kujenga nchi na kuifanya kesho yetu iwe bora zaidi kuliko jana. Alisisitiza haja ya kuendelea kuilinda itikadi ya umoja na mshikamano.

Katika hotuba yake Rais Samia hakusita kugusia masuala ya amani, akieleza kusikitishwa kwake na kuhuzunishwa na matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha, na uharibifu wa mali za Umma na za Watu binafsi kwenye baadhi ya maeneo nchini. 

Alikiri kwamba kilichotokea hakikuendana na taswira na sifa za Kitanzania. Aidha, alisema haikushangaza kuona kuwa baadhi wa vijana waliokamatwa kutokana na kadhia hiyo wametoka nje ya Tanzania.

 Kwa muktadha huo, alitoa onyo kwa wale wote waliochochea uvunjifu wa amani, akitaka watambue kuwa vurugu huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, lakini mazungumzo huzaa mshikamano. Aliagiza Kamati ya Ulinzi ya Kitaifa, na Kamati za Ulinzi za Mikoa na Wilaya, kuhakikisha maisha ya Wananchi yanarejea mara moja katika hali iliyozoeleka.







Pia, Rais alitumia fursa hiyo kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwapongeza Watanzania wote kwa imani yao, Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi, na Tume ya Uchaguzi kwa kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi kwa ufanisi usiotiliwa shaka. Aliwapongeza wagombea wenzake 17 wa urais kwa kuonyesha ukomavu wa kidemokrasia. Pongezi pia zilitolewa kwa Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, na Vyama vya Siasa kwa kumaliza uchaguzi kwa salama na amani.

Akizungumza kuhusu waangalizi wa kimataifa, Rais Samia aliwashukuru wale wote waliohudhuria kutoka Jumuiya za Kimataifa na Kikanda kama vile Umoja wa Afrika (AU), SADC, na EAC, akisema uwepo wao huongeza uhalali wa juhudi za kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya uwazi, haki, heshima, na utawala wa sheria. 

Aliwakumbusha Watanzania falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya 4R's - Kusimamia misingi ya Kuzungumza na Kuelewana (Reconciliation), Kuvumiliana (Resilience), Kubadilisha Mwelekeo (Reforms), na Kuendelea Kujenga Taifa (Re Construction/Building). Alisisitiza kuwa Serikali haitachoka wala kurudi nyuma kwenye kusimamia yote yanayohusu kujenga Umoja na Mshikamano wa Taifa.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alihitimisha kwa kutoa wito wa kuchagua hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemuko, upendo badala ya chuki, na amani badala ya vurugu. Alisisitiza kuwa Taifa letu ni bora na lina nguvu zaidi kuliko mtu yeyote. Alifafanua kwamba Masuala ya mwelekeo wa kazi za Serikali kwa miaka mitano ijayo na ufafanuzi wa kina wa dhana ya Kazi na Utu utatolewa katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments