Nyerere aliona maana ya kura hata wakati wa chama kimoja
Na Mwandishi wetu
Tunapoadhimisha Juma la Vijana na kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, ni muhimu kurudi nyuma na kutafakari maneno ya Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hata katika enzi ya mfumo wa chama
kimoja, Nyerere alisisitiza kuwa kura ni silaha ya msingi ya kila Mtanzania
kuamua mustakabali wa Taifa.
Vijana wa leo, mnao wajibu wa kujitambua na
kuchukua hatua. Fanyeni uchambuzi, simameni imara, na msiruhusu mtu yeyote
kununua dhamira yenu.
Katika hotuba zake za kuonya Taifa,
zilizojumuishwa katika mkusanyiko maarufu wa “Kilio cha Mwalimu,” Mwalimu
Nyerere alitoa onyo kali dhidi ya rushwa:"Msikubali kughilibiwa kwa
vizawadi vitakavyowapelekea kuuza haki zao... kuuza utu, heshima, amani na
uhuru wa nchi ."
Kwa maneno mengine Baba wa taifa alijua
maisha ya kila siku na kuonya vijana kwamba wasiruhusu hongo ndogo au zawadi za
muda mfupi zipoteze mamlaka yako ya miaka mitano. Baba wa taifa amesisitiza
katikia hotuba hizo kuwa Kura yako haina thamani ya fedha; ina thamani ya
mustakabali wako kwa kuepuka siasa za migawanyiko na badala yake,kuchagua
viongozi kwa msingi wa uwezo na sera zao.
Wakati wa kampeni za uchaguzi,mwaka 1975 Mwalimu Nyerere alisisitiza wajibu wa raia
kutumia haki yao ya kidemokrasia: anasema "[Waliojiandikisha wanapaswa]
kujitokeza kupiga kura [ili kuchagua] viongozi wanaofaa na wenye uwezo..."
Mwalimu aliona kura kama njia pekee ya kupata
uongozi bora. Sasa vijana wakiwa katika mfumo wa vyama vingi, chaguo lao ni
pana zaidi.
Ni kweli kuwa ikiwa Mwalimu Nyerere
alisisitiza umuhimu wa kura hata wakati kulikuwa na uchaguzi wa chama kimoja
tu, inamaanisha wewe kijana katika enzi hizi za utandawazi na uchaguzi wa vyama
vingi,Oktoba 29, 2025: Nenda Kapige Kura! Kura yako Ndiyo Sauti Yako ya
Mabadiliko!

Post a Comment