MAASAI WATIKISA NCHI! TOHARA YAENDA LIKIZO KWA AJILI YA KURA: WATANZANIA WAKATAA NJAMA ZA VURUGU!
NA MWANDISHI WETU
Katika tukio adimu, lenye uzito wa kitaifa na la
kihistoria, Jamii ya Kimaasai nchini
Tanzania imeonyesha heshima ya hali ya juu kwa Katiba na Demokrasia kwa kuahirisha zoezi lao muhimu la kimila la tohara ili kuhakikisha vijana zaidi ya
1,000 wanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huu uliotolewa na Laigwanani Mkuu, Isack Ole Kisongo Meijo, si tu tamko la uzalendo,
bali ni pigo zito kwa wale wote
wanaopanga njama za vurugu, maandamano, au mbinu za kuvuruga amani na mfumo wa
kikatiba wakati au baada ya uchaguzi.
Darasa la Uzalendo kwa Taifa
Kwa kuahirisha tukio hilo kuu la kimila, ambalo
kwa kawaida huathiri uwezo wa vijana wengi kushiriki kupiga kura, Maasai
wameweka kiwango kipya cha kuheshimu mfumo wa kidemokrasia.
Laigwanani Ole Kisongo alisisitiza wazi kuwa amani, uwajibikaji wa kiraia, na kura
ni kipaumbele kinachozidi hata matukio makuu ya utamaduni wao.
"Jamii ya Kimaasai imeonesha mfano wa kuigwa.
Huu ndio uzalendo tunaoutaka. Kura
ndiyo sauti ya maendeleo, na amani ndiyo msingi wa taifa letu,"
alikariri Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA
Amos Makalla, akipongeza hatua hiyo.
Pigo kwa Wapanga Vurugu
Kitendo hiki cha Maasai kimepokelewa kama ishara
ya wazi kwamba Watanzania wanajua
wanachotaka: Wanaamini katika mabadiliko ya kimaendeleo yanayofuata Katiba na yanayotawaliwa na amani na utulivu.
Uamuzi wa Waasai kuahirisha mila yao kwa ajili ya
kupiga kura unatoa ujumbe mkali na wa moja kwa moja kwa wale wanaopanga mbinu
za kuingia madarakani au kuleta mabadiliko kupitia njia za vurugu au maandamano
yasiyo halali: Watanzania wamechagua
sanduku la kura, siyo vurugu.
Kabla ya sherehe kuu za tohara, Maasai wameweka
neno la mwisho: Wanaheshimu mfumo wa
kidemokrasia na Katiba.
Ikiwa kabila lenye
utamaduni tajiri linaamini kwenye kura, maana yake ni kwamba njia ya amani
ndiyo njia pekee ya mabadiliko inayokubalika na Watanzania walio wengi.
Waasai wanawaonyesha Watanzania wote njia: Kura Kwanza, Vurugu Haikubaliki. Hii
inathibitisha kuwa utashi wa Taifa ni kuona maendeleo ya nchi yanaendelea
katika mazingira ya utulivu na uwajibikaji wa kikatiba.

Post a Comment